MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas amepolipongeza Jeshi la Polisi Nchini chini ya uongozi wake IGP Camilius Wambura kwa kudhibiti matukio ya kiuharifu ikiwemo vitendo vya ujambazi na uporaji ambavyo hapo awali vilikuwa vimekithiri.
Asas ameyasema hayo leo mei 29 mkoani Iringa wakati akitoa salamu za chama cha Mapinduzi CCM katika hafla ya kuvalisha nishani Maofisa, wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka mikoa mitatu ya Iringa, Dodoma na Morogoro.
Hafla hiyo imefanyika mkoani Iringa katika viwanja vya FFU na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na wazee wa kimila, ambapo mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camilius Wambura ameshiriki kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika tukio hilo,Mnec huyo ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi linastahili pongezi kutokana kazi kubwa inayofanywa ya kuthibiti vurugu zisitokee kwenye mikutano ya hadhara na maandamano yanayofanywa na vyama vya siasa nchini,ambayo hivi sasa yanafanyika katika hali utulivu na Amani.
“Nikupongeze IGP na Jeshi la Polisi kwa mambo makubwa mawili, moja matukio ya uharifu nchini yamepungua yakiwemo matukio ya majambazi kupora hayaripotiwi kama awali;
Pili vyama vya siasa vinafanya maandamano, mikutano ya hadhara bila bugudha yoyote. Tunaona kwenye vyombo vya habari huko nchi za wenzetu namna waandamanaji wanavyo nyakuliwa na polisi”Amesema.