Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
KATIBU Tawala Msaidizi Utawala na Usimamizi wa Raslimali Watu Mkoa wa Arusha, David Lyamongi, ametaka timu ya Mkoa huo kurejea na Vikombe licha ya mikoa mingine kujipanga na kujiandaa kutoa ushindani .
Lyamongi,ameyasema hayo Jana alipokuwa akifunga kambi ya uteuzi wa timu ya Mkoa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Arusha School Jijini.
Amesema kulingana na maandalizi na wachezaji walioteuliwa kuunda timu hiyo ya Mkoa,Mkoa huo utafanya vizuri katika michezo yote na utapata ushindi mkubwa na kurejea na Vikombe.
Amesisitiza kuzingatia nidhamu na Sheria ya michezo hiyo kwa kuwa hiyo ndio Siri ya ushindi na mafanikio na Uongozi wa Mkoa una Imani kubwa na timu hiyo.
Lyamongi,amewapongeza ,Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya na Jiji,Maafisa Elimu na Walimu wa michezo kwa kuandaa timu zao pia ni walezi Wazuri ambao wamewezesha kuibua Vipaji mbalimbali kwa kila mchezo.
Amehamasisha wanamichezo waliochaguliwa kuendeleza Vipaji vyao kwa kuwa siku za mbeleni Vipaji vitawasaidia kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yao.
Amewasisitiza wafanye mazoezi mara moja kwa wiki kwa kuwa ni muhimu yatawasaidia kuendeleza Vipaji vyao na kujikinga na kuambukizwa na magonjwa.
Amewaambia Wanafunzi kwamba mazoezi yanasaidia kupata uchangamfu wa mwili na kufanya vizuri katika masomo yao kwa kuwa michezo ni sehemu ya mazoezi inawanoa ubongo.
Awali Kaimu Katibu tawala msaidizi Elimu,Mkoa wa Arusha,Emmanuel Mahundo,amewapongeza Vipaji vilivyoibuliwa hasa vya kwaya na Ngoma,na akasema mashindano ya Umoja wa shule za msingi Tanzania ( UMITASHUMTA), yatafanyika kuanzia Juni 5-15 mwaka huu mkoani Tabora .
Amesema michezo itakayochezwa kwenye mashindano hayo ni pamoja na Mpira wa miguu kwa Wavulana na Wasicha, Netiboli, Mpira wa mikono ,Wavu, Riadha maalumu kwa wenye Uoni hafifu na Sanaa za mziki wa kizazi kipya.
Mahundo,amesema kuwa Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa maelekezo kwa kila Mkoa kupeleka wanamichezo 120 wenye Umri wa miaka 14 tu .
Amesema timu hiyo imepatikana kutokana na mchujo ulioanzia kwenye shule,kata na Wilaya hatimae kupata timu ya Mkoa .
Kauli mbiu inasema tujivunie mafanikio katika Sekta ya Elimu michezo na Sanaa,hima mtanzania shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.