NA ALFRED MGWENO (DODOMA),
Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, amekemea baadhi ya vyombo vya habari vinavyorusha
taarifa za upotoshaji kuhusu utolewaji wa huduma katika kivuko cha Magogoni Kigamboni na kuzua taharuki kwa wananchi wa eneo hilo.
Waziri Bashungwa, ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.
''Nitumie nafasi hii kukemea taarifa za kupotosha zinazotolewa na vyombo vya habari kuhusu vivuko
vya Kigamboni na kuzua taharuki kwa wananchi wa eneo hilo. Serikali ipo kazini na haiwezi kuhatarisha usalama wa raia wake kwa namna yoyote ile. Hivyo, niwaombe wananchi wa Kigamboni kuwa watulivu wakati Serikali inaendelea kuboresha huduma za vivuko pale Kigamboni.'' Amesema Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa ameongeza kuwa, Wizara inaendelea kuangalia utaratibu bora zaidi wa ushirikiano na Sekta Binafsi ili kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na tija kwa pande zote mbili.
Amesisitiza kuwa, matarajio ya Wizara ni kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji huduma za vivuko katika eneo la Kigamboni utaondoa kero kwa wananchi wanaotumia huduma hiyo.
''Nitoe wito kwa wawekezaji wengine wenye nia kushirikiana na TEMESA katika utoaji wa huduma
za vivuko katika maeneo mengine nchini, tunawakaribisha wawekezaji kuingia ubia (Joint Venture) na TEMESA katika matengenezo ya magari na ukodishaji wa mitambo.'' Amesema Mhe. Waziri.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Ujenziinaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi Trilioni moja, Bilioni mia saba sitini na tisa, Milioni mia mbili tisini na sita, Mia moja hamsini na mbili elfu (1,769,296,152,000.00)kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.