Katibu wa Idara ya Siasa na uhusiano wa Kimataifa (SUKI) CCM Khadija Salum katikati akizungumza na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM kuhusiana na mikakati walioiweka ya kuhakikisha kupata Idadi kubwa ya Wanawake watakao chaguliwa Majimboni Kikao kilichofanyika Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
…………….
Na Takdir Ali. Maelezo.
Chama Cha Mapinduzi kimesema hakina ubaguzi wa aina yoyote na kimetoa kipaumbele kwa Uongozi Wanawake.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mfunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis wakati uongozi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto,ulipofanya ziara ya kuhamasisha vyama vya siasa kuweka kipaumbele kwa wanawake katika utayarishaji wa Ilani za vyama vyao, kikao ambacho kimefanyika huko Ofisi kuu ya CCM Kisiwanduwi.
Amesema CCM ni chama bora, imara na cha kupigiwa mfano kwani kimeweka Viongozi 8 wanawake katika Majimbo ya Uchaguzi Zanzibar kupitia Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Aidha amesema CCM imeweka kitengo cha maadili ili kulinda haki za wanawake na yoyote atakaebainika kufanya udhalilishaji atachukuliwa hatua zinazofaa.
Hata hivyo Mbeto, amewataka Viongozi wa vyama vya siasa kufuata taratibu na Sheria zilizowekwa ili kudumisha amani na utulivu iliopo nchini kwani yanapotokezea machafuko wanaoathitika zaidi ni wanawake na Watoto.
“Matatizo mengi yansababishwa na baadhi ya Viongozi wa vyama vya siasa kwa kutotii sheria, Mfano sheria inasema ukimaliza kupiga kura ukae mbali na kituo mita mia mbili lakini wenzetu wakimaliza kupiga tu, wanahamasishana kuenda vituoni eti kulinda kura.” alisema Mbeto.
Kwa uapnde wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya jamii, jinsi na Watoto Siti Abasi Ali amesema wanarajia kufanya ziara kama hiyo kwa vyama vyote vya siasa ili waweze kuweka mikakati ya kuwanyanyua wanawake wakati wanapoandaa ilani za vyama vyao.
Aidha amesema wameamua kufanya ziara hiyo baada ya kubaini kuwa katika uchaguzi uliopita kumejitokeza matatizo mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanawake kuachwa kutokana na sababu za kisiasa.
“Katika uchaguzi uliopita baadhi ya wenzetu wameachwa kwa kutofautiana na waume zao kwa chama hasa Vijijini, mfano mwanamme anamwambia Mkewe ukaenda kupiga kura chama X ndio talaka yako. Alisema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo amewaomba Viongozi wa vyama vya siasa na wanachama kwa ujumla kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kugombania nafasi mbalimbali wakati utakapofika samamba na kuwaunga mkono ili kuweza kufikia 50 kwa 50 katika ngazi za maamuzi.
Nao baadhi ya Viongozi walioshiriki katika kikao hicho wameomba kutolewa elimu zaidi kwa wanasiasa ili waweze kujuwa majimbo hayapo kwa ajili ya wanaume pekee bali yapo kwa ajili ya mtu yoyote mwenye sifa na vigenzo vya kugombea.