Dodoma
Wizara ya Madini leo Mei 28, 2024 imekutana na wamiliki wakubwa wa viwanda vya kusafisha madini ya dhahabu nchini kwa lengo la kujadili namna ya kutatua changamoto zilizopo na kuboresha mazingira katika mnyororo mzima wa kusafisha madini ya dhahabu.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kuwa Wizara ya madini inatambua mchango wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini hivyo ili kuifanya sekta hii kuwa endelevu na yenye kuleta tija kwa wadau ni vyema kwa pamoja tukae na kujadiliana juu changamoto zilizopo na kuangalia namna ya kuzitatua kwa ushirikiano wa pamoja.
Mbibo ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha madini ya dhahabu yanaongezewa thamani nchini kupitia viwanda vya ndani hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kwa kuboresha miundombinu yote inayohusiana na sekta ya madini.
Awali, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu kufungua kikao, Kamishna wa Madini Dkt.AbdulRahman Mwanga ameeleza kuwa ajenda kubwa ni kujadiliana juu ya masuala yanayohusiana na mazingira yote usafishaji wa dhahabu kuanzia ukusanyaji, ununuzi na usafirishaji.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu kiwanda cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza (MPMR) Amin Tahir, amesema changamoto kubwa ni kutopatikana kwa malighafi ya kutosha kulisha kiwanda.
Tahir ameiomba Serikali kutunga sheria itakayowezesha madini ghafi ya dhahabu kusafishwa ndani ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani.
Naye, Mmiliki wa kiwanda cha kusafisha Dhahabu cha Geita (GGR) Sarah Masasi ameiomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuweka mazingira yatakayowezesha dhahabu inayopatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati kusafishwa ndani ya nchi.
Kikao hicho kimejumuhisha wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.