Mratibu wa Kitengo cha Ubunifu na Ujasiriamali Chuo Kikuu Mzumbe , Dkt. Irene Isibika amesema Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitengo hicho, kimekuwa kikilea mawazo ya wanafunzi wanapoingia mwaka wa kwanza hadi kubadili mawazo kutoka nadharia na kuwa uhalisia na hatimaye kuwasaidia waweze kujiajiri na kuajiri wengine baada ya kumaliza masomo yao.
Dkt Isibika ameyasema hayo leo Tarehe 27 Mei, 2024 katika maadhimisho ya wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal, jijini Tanga, ambapo wabunifu kutoka Chuo Kikuu mzumbe ni miongoni wa washiriki wa maadhimisho hayo.
Amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinawaandaa wanafunzi kwa kuchukua mawazo yao na kuhakikisha anapomaliza masomo ya darasani anatoka na ujuzi na kitu cha ubunifu ambacho kitamsaidia. Stadi za ubunifu na ujasiriamali anazozipata chuoni zimelenga kutatua matatizo kwa jamii inayotuzunguka na taifa kwa ujumla, pamoja na kufungua milango ya ajira kwa kujiajiri na/au kuajiri wengine”. Amesisitiza Dkt. Isibika.
Vilevile, Dkt. Isibika ametaja mambo ya kibunifu ya wanafunzi yaliyopo katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe. Ubunifu wa kwanza ni mfumo wa kumsaidia mkulima mdogo au mwenye mtaji mdogo kumwagilia mazao ya kisasa (automatic irrigation), kuzalisha mbegu ya mgomba kwa kutumia ndizi mbivu asilia, ufumaji wa mikoba kwa kutumia mabaki ya vitambaa vya fulana kutoka viwandani. Mfumo mwingine ni wa kuagiza chakula mtandaoni pamoja na mfumo kudhibiti maji kuingia kwenye tanki kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.
Miongoni mwa wanafunzi wabunifu kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Happiness Zabron Kaponda, kutoka Kitengo cha Ubunifu na Ujasiriamali, Mwanafunzi wa Shahada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) amesema kupitia mafunzo aliyoyapata Chuo Kikuu Mzumbe yamemsaidia kubuni mfumo unaomsaidia mkulima, ambaye alikuwa akiingia shambani na kumwagilia mwenyewe; sasa teknolojia itamsaidia kurahisisha kazi hatimaye kupata mazao mengi na yenye afya tofauti na vile angefanya kwa nguvu zake mwenyewe pekee.
Kwa upande wake Yohana Peter, Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu katika masomo ya Shahada ya Biashara Ujasiriamali na Ubunifu amekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe, kwani masomo aliyosoma na mazoezi kwa vitendo aliyofanya yamemsaidia kubuni mfumo wa kusaidia mwanafunzi au mteja yoyote kuagiza chakula kwa watoa huduma wa chakula bila kukutana na mtoa huduma huyo na kupata huduma anayohiataji.
Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa vyuo na taasisi zinazoshiriki maonesho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yenye Kaulimbiu: Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa Uchumi Shindani yalioanza Mei 25 jijini Tanga na kufungwa rasmi leo Mei 27 na Waziri wa Elimu Sanyansi na Teknolojia Dkt. Aldof Faustine Mkenda.