Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis akizungumza katika Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa na Waandishi wa Habari kuhusiana na Operesheni iliofanywa na Jeshi la Polisi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali wa Makundi ya Kihalifu katika mkoa wamjini Magharibi Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka akizungumza katika Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa na Waandishi wa Habari kuhusiana na Operesheni iliofanywa na Jeshi la Polisi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali wa Makundi ya Kihalifu katika mkoa wamjini Magharibi Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa Zanzibar Kebo Tv Amour Khamis akiuliza maswali katika Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa kuhusiana na Operesheni iliofanywa na Jeshi la Polisi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali wa Makundi ya Kihalifu katika mkoa wamjini Magharibi Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa Zanzibar Leo Mwajuma Juma akiuliza maswali katika Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa kuhusiana na Operesheni iliofanywa na Jeshi la Polisi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa mbalimbali wa Makundi ya Kihalifu katika mkoa wamjini Magharibi Zanzibar. (PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR)
………….
Na Khadija Khamis- Maelezo, Zanzibar 28/04/2024.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema jumla ya watuhumiwa 251 wamekamatwa kufuatia operesheni maalum ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu hapa Nchini.
Ameyasema hayo huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Vuga wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa 22 wamekamatwa na mapanga na vifaa vya kuvunjia nyumba, 20 wamekamatwa kwa makosa ya unyan’ganyi, kujeruhi na kushambulia, 6 kwa makosa ya wizi wa pikipiki wakiwemo mafundi wa pikipiki wanaopokea mali za wizi na watuhumiwa 203 wamekamatwa kwa makosa ya uzembe na ukorofi.
Aidha, amefahamisha watuhumiwa wote waliokamatwa katika operesheni hiyo watafikishwa katika vyombo vya sheria na majalada yao yemeshafunguliwa kwa ajili ya kufikishwa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ili kuendelea na taratibu nyengine za kisheria.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema operesheni hizi zitakua endelevu katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi hadi kuhakikisha makundi hayo ya vijana wanaotumia silaha za jadi yamedhibitiwa kabisa kwa mashirikiano ya jeshi la polisi na vyombo vyengine vya ulinzi.
Pamoja na hayo, Amewaasa vijana ambao wanajiingiza katika matendo hayo kwamba Serikali haitoacha vitendo hivyo viendelee itapambana hadi kuhakikisha makundi haya yanatokomea.
“nitoe indhari kuwa Serikali ya Mkoa pamoja na Jeshi la Polisi halitakuwa tayari kumuachia kijana yoyote yule atakaebainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu, ”amesema Mkuu wa Mkoa.
Amewataka wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya ulinzi hasa hasa jeshi la polisi kwa kuwapa taarifa sahihi za vikundi vya watu ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao ili kuweza kudumisha amani na utulivu kwenye mkoa.
Nae Mkuu wa Wilaya Magharibi ‘B’ ambae pia ni Kaimu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Hamida Mussa Khamis ameishukuru Kamati ya Usalama wa Mkoa kwa kuendelea kuzisimamia Wilaya zao na kutoa muongozo wa jinsi ya kukabiliana na uhalifu huo.
Akielezea wilaya yake amesema kuwa bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa na vikundi vya uhalifu ikiwemo Kinuni Kwarara Hawai pamoja na Mchikichini.
Kwa upande wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ACP Richard Thadei Mchomvu amesema operesheni huo imefanyika kwa aina yake jambo ambalo limesaidia kuleta mafanikio ya kuwakamata wahalifu.
Hata hivyo amewapongeza masheha na wananchi kwa mashirikiano yao waliyoyatoa jambo ambalo limeweza kufanikisha zoezi hilo
Mali zilizookolewa katika Operesheni hizo ni pikipiki 14, Televisheni 4 , simu 16, mifuko ya saruji 4, Tiles box 5, Viatu vya raba pair 6 , pasi za umeme 3, frame 44 za pikipiki aina ya klick na vespa pamoja na N’gombe 2.
Sambamba na hayo operesheni hiyo yameweza kukamata pombe za kienyeji lita 240 bangi gram 32, mitambo mitatu ya kutengenezea pombe za kienyeji pamoja na kukamatwa wanawake sita wanaojishughulisha na pombe hiyo sambamba na kuvunjwa vijiwe (maskani) 60 za vikundi vya vijana.