CHAMA cha Mawakili wa Serikali Tanzania kimewaahidi wananchi mkoani Njombe kuwa watatumia ujuzi wao wa sheria kutatua kero mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign).
Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Amedeus Shayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya huduma ya msaada wa kisheria iliyofanyika Halmashauri ya Mji wa Njombe.
“Mkoa wa Njombe ni mkoa ambao umefikiwa na kampeni ya Mama Samia, wananchi wa Njombe wana matatizo mtambuka na sisi tumeleta Njombe taaluma yetu ya sheria na tunawakaribisha wananjombe wote kutoka wilaya zote kupata huduma” amesema Shayo.
Naye Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School), Dk. Clement Mashamba amesema wamefika Njombe kushirikiana na wadau wengine ili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria.
“Sisi ni Taasisi ya mafunzo ya kisheria hivyo kutoa msaada wa kisheria ni sehemu ya kazi yetu lakini pia kwenye taasisi yetu tuna kituo cha huduma ya msaada wa kisheria ambacho kinatoa huduma hizi bure kwa wananchi,” amesema Dk. Mshamba.
Aidha Dk. Mashamba amebainisha kuwa taasisi hiyo inatoa kozi ya Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) kwa ngazi ya Cheti na Diploma ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wataalamu wa masuala ya sheria wanaongezeka na huduma zinasogea karibu zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.