Na. WAF, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Mfumo wa kulipia Bima za watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na Timiza ambapo wanajiunga kupitia wazazi wao.
Dkt. Mollel amebainisha hayo leo Jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya bungeni katika bunge la 12 mkutano wa 15 kikao cha 34.
Dkt. Mollel amesema kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utawezesha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo Watoto kupata huduma za Afya kwa urahisi pasipo kuwa na vikwazo.
“Nitoe rai kwa Waganga wafawidhi wa Hospitali za Rufaa nchini kuhakikisha wanawapokea watoto wanaotoka katika maeneo ya hospitali zilipo na kuwapatia Huduma”, ametoa wito Dkt. Mollel
Dkt. Mollel ameeleza kuwa Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya Ukamilishaji wa Jengo la Mama na Mtoto, wodi ya Watoto na wodi ya wanaume katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi lenye sehemu 2 ambazo ni msambamba A na B.
Aidha eneo la msambamba A limekamilika kwa 98% na tayari linatumika kwa huduma za wagonjwa wa nje na huduma za Radiolojia na,eneo la msambamba B limefikia asimia 20 na ujenzi unaendelea.
Katika hatua nyingine Serikali imefanya uzinduzi wa Kampeni ya Mtu ni Afya kwa awamu ya pili ambayo inahimiza kuhusu kujengo vyoo bora, lishe bora, udhibiti wa taka, udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza sambamba na unawaji wa mikono kwa maji na Sabuni.
Dkt. Mollel ametoa wito kwa Wabunge na Watanzania kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono ili kuendelea kuchukua tahadhari juu ya magonjwa mbalimbali.
Kampeni hii imezinduliwa tarehe 9.5.2024 na Mheshimiwa Daktari Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutekelezwa kwake kutawezesha kudhibiti magonjwa ambukizi katika jamii.