Geneva Uswisi,
Tanzania imepongezwa kwa kuwa na mikakati yenye kulenga ustahimilivu na uendelevu wa mifumo ya afya na mwitikio wa UKIMWI ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa katika kudhibiti ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030
Hayo yamebainishwa kupitia kikao kilichowakutanisha kwa pamoja ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe pamoja na viongozi waandamizi kutoka mashirika ya kimataifa ya UNAIDS, Global Fund, PEPFAR na wadau wengine wa kimataifa kwenye kikao cha kujadili jitihada zinazochukuliwa na Tanzania katika uendelevu wa Mwitikio wa kudhibiti UKIMWI ifikapo na baada ya mwaka 2030.
“Tanzania imeendelea kuongeza jitihada kuimarisha mifumo ya afya kwa kusogeza huduma za afya ikiwemo za VVU/UKIMWI karibu na wananchi kwa kujenga vituo vipya vyenye kutoa huduma za kinga, uchunguzi, tiba na utengemao” amesema Dkt. Magembe huku akiongezea kuwa Serikali imeendelea kuajiri watumishi wapya hususani katika vituo vya afya vilivyopo vijijini.
Dkt. Magembe alisema kuwa dhana ya uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI imedhihirika kwa kuanzisha Mfuko wa UKIMWI mwaka 2001 ambapo Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka za kutekeleza afua kinga za kuzuia maambukizi mapya ya VVU.
Washirika wa Kimataifa wameipongeza Tanzania kwa jitihada za kudhibiti UKIMWI pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo endelevu vya kuhakikisha malengo ya kudhibiti ugonjwa huo yanafikiwa ifikapo mwaka 2030.
Katika kikao hicho Dkt Magembe aliambatana na Dkt Charles Mahera, Naibu Katibu Mkuu (Afya), Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Dkt Catherine Joachim, Mkuu wa Program, Wizara ya Afya.