Na Mwandishi wetu, Haydom
WAJAWAZITO 600,000 wa mikoa mitano nchini watanufaika na mradi wa kitita cha uzazi salama (SBBC) utakaoboresha huduma za mama na mtoto utakaopunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Wanawake hao kutoka mikoa mitano nchini ya Manyara, Geita, Tabora, Shinyanga na Mwanza, watanufaika kupitia mradi huo wa kitita cha uzazi salama (SBBC).
Msimamizi wa mradi huo Dk Pascal Mdoe, ambaye ni mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya kilutheri ya Haydom amesema jamii ya mikoa hiyo mitano itanufaika kupitia mradi huo wa kitita cha uzazi salama.
Dk Mdoe amesema kupitia mradi huo wanawake hao wajawazito wa mikoa hiyo watanufaika kwa uzazi salama na kupunguza vifo na watoto chini ya miaka mitano.
Amesema kwa muda wa miaka miwili wanawake hao watanufaika na pia watoa huduma 4,000 watawezeshwa kielimu na vifaa hivyo jamii kubwa kufikiwa na mradi huo.
“Natoa wito kwa wajawazito wasijifungulie nyumbani ila wafike kwenye kliniki ya uzazi na isipungue mara nne ili watoa huduma wawangalie na wabaini kama wana changamoto,” amesema Dk Mdoe.
Hata hivyo, amesema wataalamu wa sayansi kutoka baadhi ya nchi ikiwemo Nigeria, Ethiopia na Kenya wamefika Haydom kwa ajili ya kujifunza namna mradi huo ulivyosaidia jamii nchini.
Kaimu mganga mkuu wa serikali, Dk Ahmad Makuwani amesema kupitia mradi huo hatua kubwa zimefikiwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Dk Makuwani amesema awamu ya pili ya mradi huo itanufaisha zaidi jamii mojamoja wakiwemo watoa huduma, wanawake na watoto kwani vifo vya uzazi vimepungua mno.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Damas Kayera amesema mradi huo kwenye awamu ya kwanza kulikuwa na vituo sita vya kutoa huduma na kuwanufaisha wanawake wa eneo hilo.
Dk Kayera amesema wameona matokeo makubwa ya mradi huo kwani watumishi walipata vifaa vya kujifunzia, mafunzo na kujengewa mfumo na kuboresha huduma.
Mmoja kati ya wanawake waliojifungua kwenye hospitali ya Haydom, Elizabeth Bea ameushukuru mradi huo kwani umepunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto.
“Kitita cha uzazi salama kimekuwa na manufaa makubwa kwetu sisi wanawake, watoto na jamii kwa ujumla, hivyo tuunge mkono mradi huu,” amesema.