Na. Zillipa Joseph, Katavi
Miili ya watu waliokufa kwa ajali ya mtumbwi kupinduka katika kitongoji cha Lunguya kijiji cha Mwamapuli Halmasahuri ya Mpimbwe wilaya ya mlele mkoani katavi; imefikia minne baada ya miili mingine mitatu kuopolewa na jeshi la zimamoto na uokozi wakishirikiana na wananchi.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Katavi Inspekta Lilian Wanna amesema miili hiyo imekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko.
Aidha Inspekta Lilian ametaja sababu za ajali hiyo kuwa ni mtumbwi huo kuzidiwa uzito baada ya kubeba magunia kumi ya mpunga na abiria 14 waliokuwa wakisafirisha mpunga huo kutoka mashambani kuleta kijijini.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema maji yanayopatikana katika bonde hilo yametoka mto Kavuu baada ya mto huo kufurika na kuiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliwaagiza viongozi wa eneo hilo kusimamia usafirishaji wa mizigo na abiria ili kuzuia madhara mengine yasijitokeze.
Katika ajali hiyo ilyotokea Mei 24 majira ya saa 12:30 jioni watu saba kati ya 14 waliokuwa wakisafiri katika mtumbwi huo walipoteza maisha baada ya mtumbwi kupinduka.