Na Mwandishi Wetu, Morogoro
UAMUZI wa RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan kuibeba kwa uzito ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, imemwibua MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara,Abdulrahman Kinana ambaye amesema hatua hiyo inadhihirisha umakini, uwezo na Nia safi ya Rais kuwainua wanawake kiuchumi.
Kinana amesema kampeni ya nishati safi iliyoanzishwa na Rais Dk. Samia inalenga kumtua mwanamke mzigo wa kuni kichwani na kumpa muda mwingi wa kujikita katika shughuli za kukiletea maendeleo.
Akizungumza mbele ya wanachama wa CCM katika Kata ya Ngerengere, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Kinana amesema uamuzi huo unakusudia kusaidia kuwainua wanawake.
“Nimeona mitungi ya gesi ambayo nitaikabidhi na uwepo wa mitungi hii ni matokeo ya sera na ubunifu kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Mwaka jana Rais Samia alianzisha mchakato wa kuwatua akina mama mzigo wa kuni, kaanzisha mradi wa nishati safi na salama,”” amesema.
Kinana ametaka kampeni hiyo iendelee kuungwa mkono kwa uzito mkubwa kuhakikisha lengo lililokusudiwa linatimia.
Mbunge wa jimbo hilo Hamisi Taletale alitumia mkutano huo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na kukabidhi mitungi 800 ya gesi ya Kampuni ya Oryx na majiko yake.