Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akizungumza katika Mkutano wa 30 wa Wahandisi Washauri Barani Africa (FIDIC AFRICA), jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, (kulia) akiwa na Profesa maarufu nchini Kenya, Patrick Lumumba (kushoto) katika Mkutano wa 30 wa Wahandisi Washauri Barani Africa (FIDIC AFRICA), jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa Mkutano wa 30 wa Wahandisi Washauri Barani Africa (FIDIC AFRICA), jijini Dar es Salaam. Mkutano huo wa siku Tatu umebebwa na kauli mbiu ‘Ubunifu na Maendeleo ya Miundombinu, kwa ajili ya miradi Endelevu’.
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (WaTatu kushoto waliokaa) na viongozi wa Umoja wa Wahandisi Washauri Barani Africa (FIDIC AFRICA), katika Mkutano wa 30 wa Wahandisi Washauri hao , jijini Dar es Salaam.
……………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesisitiza Umoja wa Wahandis Washauri Africa (FIDIC AFRICA) kuangalia namna ya kutengeneza Wahandisi Washauri wazuri wa Africa ikiwemo Tanzania ili miradi inayotekelezwa nchini kutekelezwa na wazawa wenyewe badala ya wataalam kutoka nje ya nchi.
Kasekenya amezungumza hayo Mei 27, 2024 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa 30 wa Wahandisi Washauri Barani Africa (FIDIC AFRICA), jijini Dar es Salaam wenye kauli mbiu ‘Ubunifu na Maendeleo ya Miundombinu, kwa ajili ya miradi Endelevu’.
“Naamini FIDIC watatumia Kongamano hili kwenda kujibu changamoto mbalimbali zinazowakabili wataalam hawa na kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo ukosefu wa vifaa, mitaji au kutokufanya kazi kwa ushirikiano”, amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya ametoa rai kwa FIDIC kutengeneza mazingira mazuri kwa wahandisi washauri ikiwemo kuwajengea uwezo wataalam hao ili kukuza taaluma yao na kuendana na kasi ya mabadiliko Teknolojia na hivyo kukuza ushindani ndani na nje ya nchi.
Kadhalika Kasekenya, amewaelekeza wataalam hao kutumia ushiriki wao katika mkutano huo kuishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali ikwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika Sekta ya Ujenzi.
Naye, Rais wa Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania (ACET), Mhandisi Chedi Masambaji amesema kuwa Mkutano huo utatoa fursa ya kupata mrejesho na maoni kutoka kwa wataalam mbalimbali ulimwenguni kuhusu miundombinu.
Mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Nigeria, Misri, Senegal, Msumbiji na mwenyeji Tanzania yameshiriki katika Mkutano huo, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu Taaluma yao na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi.