*Yapongeza umakini katika udhibiti
Na Mwandishi Wetu.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), imetoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu ukokotoaji wa bei za bidhaa za mafuta nchini.
Elimu hiyo imetolewa tarehe 27 Mei 2024 katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma ambapo Wabunge hao walipata nafasi ya
kujifunza namna tofauti za ukokotoaji wa bidhaa ya mafuta nchini.
Akizungumza, wakati wa utoaji wa elimu hiyo kwa Wabunge, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi kutoka EWURA, Bw. Msafiri Mtepa amesema bei za mafuta nchini hupangwa kwa kutumia kanuni ya kupanga bei za nafuta ya mwaka 2022 ambapo kanuni hiyo imekuwa ikifanyiwa marekebisho na mabadiliko mbalimbali yanayohusu upangaji wa bei za mafuta hapa nchini.
Aidha, amesema bei za mafuta zinapangwa kila mwezi na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali baada ya kupitishwa na Bodi ya EWURA ambapo utayarishaji wa kanuni hizo hushirikisha wadau wote muhimu wakiwemo Wananchi.
Pia Ametaja sababu zinazosababisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini kuwa ni pamoja na madhara ugonjwa wa Corona ambao umesababisha kupungua kwa hifadhi ya mafuta duniani, hali ya usafirishaji wa mafuta kuwa mbaya na kupungua mahitaji ya mafuta pamoja na thamani ya fedha kushuka kutokana na kuanza kwa Vita ya Urusi na Ukraini.
Kwa Upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe
Ng’enda ameipongeza Serikali kwa umakini wake katika kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini pamoja na udhibiti wake.
Pia ameshukuru kwa elimu hiyo ambayo imewaongezea uelewa kuhusu sekta husika.upatikanaji wa mafuta nchini.
Pia, ameitaka EWURA kuendelea kusimamia vizuri mwenendo mzima wa upatikanaji wa mafuta, kusimamia bei za mafuta na kudhibiti upandaji wa bei ya bidhaa hiyo nchini.
Kwa Upande wake Naibu Waziri Wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Wizara itafanyia kazi ushauri wote uliotolewa na kamati ili kuweza kuboresha huduma ya upatikanaji wa mafuta na udhibiti wa bei ya mafuta nchini.