Watu saba kati ya 14 waliokuwa wakisafirisha magunia ya mpunga kwa kutumia mtumbwi katika kitongoji cha Lunguya katika kijiji cha Mwamapuli halmashauri ya Mlele mkoani Katavi wamepoteza maisha baada ya mtumbwi huo kupinduka.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Katavi Inspekta Lilian Wanna amesema tukio hilo lilitokea mei 24 majira ya saa kumi na mbili jioni.
Alieleza kuwa watu hao walikuwa wakitoa mazao yao shambani na kuyaleta kijijini wakati ajali hiyo ilipowakuta.
Inspekta Wanna amesema wanaendelea na kazi ya uokoaji licha ya kuwa bonde hilo kuwa changamoto ya mamba na viboko.
Nuhu Bahati amepoteza ndugu zake wawili akiwemo mtoto wa miaka 14, anasema ndugu zake walimwacha kambini kwa lengo la kuwahi kwenda kuchaji simu zao.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi mkoani katavi ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo bi. Mwanamvua Mrindoko alifika kijijini hapo kutoa pole kwa wafiwa; na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la zimamoto katika kazi ya uokoaji.