Naibu waziri mkuu Dokta Dotto Mashaka Biteko ameagiza kushughulikiwa kwa haraka kwa migogoro mbalimbali inayojitokeza katika jamii badala ya kusubiri mpaka maafa yatokee kwa wananchi.
Awali Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka na Mbunge wa Jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika Wamesema wanatarajia kuona kampeni hiyo inakwenda kutatua kero za wananchi ambao wamekosa huduma za kisheria kutokana na kukosa fedha.
Waziri wa Maendeleo ya jamii Jinsia Wanawake na makundi Maalumu Dokta Dorothy Gwajima amesema ripoti zinaonesha kuongezeka kwa ukatili ambapo katika kipindi cha Januari Disemba mwaka 2022 watoto 12163 walifanyiwa ukatili ikiwa hadi sasa jumla ya watoto 15301 wamekatili jambo ambalo litaendelea kudhibitiwa kikamilifu huku wanaume wakitakiwa kujitokeza kueleza maswahibu wanayokutana nayo toka kwa wake zao.
Naye waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dokta Pindi Chana amesema Rais Samia ameleta kampeni hiyo ili kuwasaidia wananchi wanaokosa msaada wa kisheria.
Katika mkoa wa Njombe Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inakwenda kuhudumu katika kata 60 kwa siku kumi ikiwafikia wananchi pasina gharama yoyote.