Tanzania yaungana na nchi wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) kupitisha na kusaini Mkataba wa kihistoria wa kimataifa kuhusu Miliki Ubunifu, Rasilimali za Kijenetiki na Maarifa ya Jadi.
Mkataba huo unalenga kulinda haki za wenyeji asilia na jamii za kijadi katika kuhakikisha matumizi ya rasilimali za kijenetiki na maarifa ya jadi katika tafiti na vumbuzi yanaleta faida kwa jamii hizo.
Mkataba huo wa kihistoria na wa aina yake umejadiliwa kwa takribani miaka 25 na nchi wanachama wa WIPO kabla ya kupitishwa rasmi tarehe 24 Mei, 2024 katika Mkutano wa Kidiplomasia uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Geneva, Uswisi.
Mheshimiwa Dkt. Abdallah S. Possi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa Jijini Geneva aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa Kidiplomasia uliopitisha Mkataba tajwa, na kusaini Mkataba kwa upande wa Tanzania.
Walioshuhudia hafla ya utiaji saini mkataba huo ni Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji wa BRELA, Bw. Twalib Njohole, Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea kutoka Wizara ya Kilimo, Bi. Loy Mhando, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA na Bi. Zulekha Fundi, Afisa Mambo ya Nje kutoka Ubalozi wa Tanzania Geneva.
Baada ya Mkataba huu kuridhiwa na nchi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) watakuwa na jukumu la kuhakikisha waombaji wa ulinzi wa Vumbuzi kupitia Sheria za Hataza wanafichua taarifa za mahali zilipopatikana rasilimali za kijenetiki na maarifa ya jadi yaliyotumika katika tafiti na vumbuzi husika.
Vilevile, kufuatilia matumizi ya rasilimali hizo zinazopatikana hapa nchi ambazo watafiti na wavumbuzi kutoka nchi nyingine wanazitumia katika tafiti na vumbuzi zao ili kuhakikisha wamiliki wa rasilimali hizo hapa nchini wanapata faida zitakazotokana na matumizi ya rasilimali hizo.
Mkataba huu utaanza kutumika rasmi siku 30 baada ya nchi 15 kuwasilisha nyaraka za uridhiwaji wa Mkataba huo katika Ofisi za WIPO.