Mkuu wa wilaya ya Iringa Komredi Kheri James amewashauri na kuwahimiza vijana wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Iringa Mjini, kujenga mshikamano miongoni mwao na kuwajibika ipasavyo katika ujenzi wa jumuiya na shughuli zao za uzalishaji mali.
Komredi Kheri James ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu zake katika kikao Cha Baraza la vijana wa Chama Cha Mapinduzi kilicho fanyika katika Ofisi za CCM wilaya ya Iringa Mjini.
Akizungumza katika kikao hicho Kheri James ameeleza kuwa umoja na mshikamano ni silaha muhimu sana katika safari ya kuyafikia mafanikio, kwahiyo ni muhimu vijana wakaendelea kushikama na kushirikiana katika kusimamia ajenda zinazo wagusa vijana wote kwa ujumla.
Aidha Kheri James amewahimiza vijana kuwajibika kikamilifu katika majukumu waliokabidhiwa ndani ya Jumuiya na kuwajibika zaidi katika kuzitumia fursa zilizipo ndani ya wilaya ili kujijenga kiuchumi na kijamii.
Pamoja na mambo mengine Kheri James amewahimiza vijana wa Chama Cha Mapinduzi kuwa mawakili wa hoja za vijana wenzao wote ili hoja na ushauri wa vijana na mambo yao viwasilishwe katika mamlaka zinazo husika kwa wakati na hatua zichukuliwe kwa wakati.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na viongozi wa Chama, Jumuiya na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana katika wilaya ya Iringa.