………………..
WANANCHI wa Kijiji cha Sumve,wilayani Kwimba wamechanga fedha za kununua eneo na kuchangia nguvu zao kujenga Kituo cha Afya Budushi ili kutatua changamoto ya kusafiri umbali wa kilometa 14 kwenda kupata huduma ya matibabu katika Kituo cha Afya Koromije.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kwimba, Happiness Msanga ameiiambia Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza, leo ilipokagua mradi huo ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
“Kituo hiki cha Afya Budushi, kimegharimu sh. milioni 321 za mapato ya ndani,nguvu za wananchi zimetumika kuchimba mitaro na kusomba mchanga ambapo jumla ya mchango wao ni sh.milioni 16 zikiwemo sh. milioni nane za kununua eneo kilipojengwa kituo,”amesema.
Msanga amesema miundombinu baadhi ya kituo hicho iliyokamilika na na kuwezesha wananchi kuanza kuhudumiwa , miundombinu hiyo ni jengo la wagonjwa wan je (OPD), wodi mbili za wanaaume na wanawake, kichomea taka,vyoo huku jengo la maabara lenye thamani ya sh. milioni 356 likijengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Amesema kukamilika kwa kituo hicho cha Afya Kadushi kumewezesha wananchi kupata huduma karibu na kuwaondolea adha ya kusafiri umbali wa kilometa 14 kwenda kupata huduma za matibabu Kituo cha Afya Koromije na kurudi.
Pia,kituo kimepunguza msongamano katika kituo cha Afya Koromije na Hospitali Teule ya Sumve (DDH), hivyo mikakati ni kujenga chumba cha kuhifadhi maiti na nyumba za watumishi kwa kushirikiana na TASAF.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kwimba, Saban Lushu,amesema wananchi wa Sumve wana umoja wa pekee katika kusukuma maendeleo na kuwapongeza kwa kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha huduma za afya.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’,ameishukuru Halmashauri ya Kwimba na TASAF kwa utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria unaolenga kutoa huduma za tiba kwa wananchi.
Pia amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Sumve kwa kuchangia nguvu zao na fedha za kununua eneo la kujenga kituo cha afya na kuchimba msingi wapate huduma karibu.
Smart ameiagiza halmashauri kutumia mfumo wa kielektroniki kwa malipo ya huduma badala ya stakabadhi za karatasi,kuepuka mapato ya kituo hicho kuvuja.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakiwemo Abel Elias wa kijiji jirani cha Bumengeji,wamesema kujengwa kwa kituo hicho cha Kadushi kumewakomboa sasa watapata huduma karibu.
“Umbali wa kutoka Bumengeji kwenda kufuata huduma za afya Koromije umbali wa kilometa 15 ilikuwa changamoto kwa wananchi,sasa tutahudumiwa karibu, kimewasaidia wananchi kwa kiwango kikubwa,”amesema na kuongeza kuwa maabara ikikamilika itasaidia kuptikana kwa huduma ya vipimo.