Viongozi wa Taasisi mbalimbali nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya uongozi pamoja na kutengeneza mazingira rafiki ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ya jambo ambalo litasaidia kutengeneza msingi katika ulinzi wa amani na usalama wa Afrika.
Akizungumza katika Kongamano maalumu lililoandaliwa na Uongozi Institute kwa ajili ya kujadili masuala ya ulinzi na Usalama Afrika, lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kamishna wa Masuala ya Kisiasa, Ulinzi na Usalama wa Umoja wa Afrika (AU), Balozi Bankole Adeoye, amesema kuna haja Baraza la Usalama la Afrika kuwashirikisha vijana katika masuala mbalimbali ili kuleta tija.
Balozi Adeoye amesema kuwa amani inayotakiwa Afrika ni ile itakayowezesha vijana na wanawake kuwezeshwa kwa kila namna, huku akisisitiza amani hiyo itajengwa kwa kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto Afrika.
“Nani anapaswa kuwa kiongozi, nani anapaswa kushauri, nani anapaswa kuwa mfano wa amani Afrika tunapaswa kuwa na taasisi imara ili tuwe na amani tunayoitaka Afrika,” amesema.
Nae Balozi mstaafu wa Tanzania, Brigedia Jenerali mstaafu Paul Mella, amefafanua kuwa hivi sasa mahitaji ya ulinzi wa usalama yanaongezeka kwani machafuko ya nchi moja na nyingine yanaongezeka.
Amesema kuna changamoto maeneo mengi kuhusu walinzi wa kulinda amani katika nchi za afrika, hivyo juhudi za pamoja zinahitaji ikiwemo kuwa vikosi imara pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa.
Ameeleza kuwa jukumu la kulinda amani na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa salama ni jukumu la kila mmoja na sio vyombo vya ulinzi na Usalama.
Brigedia Jenerali mstaafu Paul Mella amesema kuwa katika maeneo ambayo kumekuwa na changamoto za kiusalama kumekuwepo na taasisi mbalimbali ambazo zote zinashiriki katika kulinda masuala ya ulinzi na usalama.
Mhadhiri wa Masomo ya Kimkakati katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Profesa Eginald Mihanjo, amesema kuwa ulinzi na amani kinashabihiana na uwezo wa kiuchumi wa wananchi.
Amesisitiza kuwa msingi wa uchumi ni wananchi hasa vijana baada ya kuhitimu elimu ya juu wawe katika ajira, hivyo amesema ni vigumu nchi husika kuwa na amani kama vijana wengi hawana ajira.
“Kufikia mwaka 2050 zaidi ya asilimia 50 ya watu wa Afrika watakuwa vijana na inawezekanaje kuwa na amani iwapo wanataka kuingia kusaka fedha na hawana ajira,” amesema.
Pamoa na hayo Baraza la Usalama la Afrika limetimiza miaka 20, hivyo wasomi wa kada mbalimbali pamoja na wabobezi wa masuala ya ulinzi, Usalama pamoja na Diplomasia katika Bara la Afrika wameeleza iko haja kwa Bara hilo kuhakikisha inaendelea kuweka mikakati itakayoshirikisha makundi yote yakiwemo ya vijana kwani takwimu zinaonesha mwaka 2050 nusu ya watu wa Afrika watakuwa chini ya miaka 25.