Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kizuka Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma wakipita katika Daraja la Mto Njoka lililojengwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA) linalounganisha kijiji hicho na vijiji mbalimbali vya wilaya ya Mbinga na nchi jirani ya Msumbuji.
Muonekano wa Barabara la lami ya Kifagilo-Magingo Halmashauri ya Madaba wilayani Songea ambayo ujenzi wake umekamilika.
Kaimu meneja wa wakala wa Barabara za mijini na vijijini(TARURA)wilayani Songea Mhandisi Davis Mapunda kushoto, akizungumza na baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Madaba juu ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara za lami katika maeneo mbalimbali.
……
Na Mwandishi wetu, Songea
MTANDAO wa Barabara mkoani Ruvuma una urefu wa takribani kilometa zipatazo 6,297.25 ikiwemo kilometa 2,166.62 za Barabara zinazosimiwa na TANROADS na kilometa 4,130.63 zinasimamiwa na TARURA).
Kutokana na hali ya jiografia ya mkoa huu,usafiri wa Barabara unatajwa kuwa ndiyo njia kubwa inayotumiwa kwa usafiri na usafirishaji wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 80 hadi 90 ya abiria na mizigo hutumia Barabara ndiyo maana Serikali imekuwa ikifanya jitihada mwaka hadi mwaka za kuimarisha na kuboresha miundombinu ya Barabara ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuzilinda ziweze kutumika kwa muda mrefu.
Kaimu meneja wa wakala wa Barabara za mijini na vijijini(TARURA) Mhandisi Silvanus Ngonyani anasema,Serikali inaendelea na juhudi ili kuufanya mtandao wote wa Barabara kupitika kwa misimu yote kwa kutenga fedha mwaka hadi mwaka.
Ngonyani anasema,kwa ujumla Barabara za mkoa wa Ruvuma zinazohudumiwa na TARURA zipo katika hali nzuri kwa wastani wa asilimia 57.80 na kilometa 3,015.59 za mtandao wa Barabara zilizobaki sawa na asilimia 42.20 hupitika kikamilifu wakati wa kiangazi tu.
“Serikali imeendelea kuiongezea TARURA mkoa wa Ruvuma fedha kutoka Sh.7,644,050,642.00 mwaka 2020/2021 hadi Sh.22,498,956,998.23 sawa na asilimia 194.3 kwa mwaka 2023/2024 kwa ajili ya kuboresha mtandao wa barabara”anasema.
“Fedha hizi zimetoka serikali kuu na fedha za Tozo ya Sh.100 kwa kila lita moja ya mafuta(dizel na petrol) na fedha za mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kujenga,kukarabati na kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara”anasema.
Anasema kupitia ongezeko hilo TARURA mkoa wa Ruvuma, inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kufungua barabara mpya ili kufika kusiko fikika na kuboresha barabara zilizopo ili kufika wakati wote.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za mapato ya ndani na ushuru wa maegesho anasema,katika kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuboresha barabara kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu wa kilometa 30.435 sawa na asilimia 33.78 ya uongezeko la barabara za lami.
Kwa mujibu wa Ngonyani,kabla ya mwaka 2023/2024,barabara za lami zinazohudumiwa na Tarura katika mkoa wa Ruvuma zilikuwa kilometa 94.095 mwaka 2021 lakini sasa kuna jumla ya kilometa 124.53.
Kwa upande wa barabara za changarawe Ngonyani anasema,awali kulikuwa na kilometa 749.637 lakini kutokana juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kupitia TARURA barabara hizo zimeongezeka hadi kufikia kilometa 1,478.382 sawa na asilimia 50.7.
Aidha anasema,wamefanikiwa kupunguza Barabara za udongo kwa asilimia 13.7 ambapo mwaka 2021 kulikuwa na kilometa 6,302.471 lakini hadi mwishoni mwa mwezi Machi 2024 kuna kilometa 5,543.287 tu za Barabara za udongo.
MADARAJA.
Kwa mujibu wa Ngonyani,katika kipindi hiki wamejenga jumla ya madaraja 206,makalavati 531,madrifti 14,mifereji mita 6,912,kufungua barabarani mpya kilometa 392 na taa za barabarani zimeongezeka kutoka 340 hadi 383 sawa na asilimia 12.6.
Pia amesema,barabara zilizo katika hali nzuri nazo zimeongezeka kutoka kilometa 1,391.453 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kilomita 2,393 mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na asilimia 172.05.
Anasema,barabara zilizo katika hali ya wastani nazo zimeongezeka kutoka kilometa 1,572.083 mwaka 2020/2021 na kufikia kilometa 2,128.237 kwa mwaka 2023/2024 ambayo ni sawa na asilimia 35.38.
Vile vile anasema,barabara zilizo katika hali mbaya zimepungua kutoka kilometa 4,182.667 mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka kufikia kilometa 2,624.011 mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na asilimia 59.4.
Anataja kazi zilizofanyika kupitia fedha hizo ni kuunganisha huduma za usafiri wa barabara za ndani ya Mkoa,kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya moto, kupunguza muda wa kusafiri na wakala kufanikisha malengo na maono yake.
Hata hivyo anasema,katika kutekeleza majukumu yake Tarura inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo wananchi kulima kwenye hifadhi za barabara,kuiba na kuharibu alama za barabara na mabomba ya daraja,wakandarasi kukosa mitambo ya kufanyia kazi pamoja na mitaji.
Changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti ya matengenezo ukilinganisha na ukubwa wa mtandao wa barabara,mvua nyingi zilizonyesha,upungufu wa majengo ya umma kwa ajili ya shughuli za ofisi hususani katika wilaya ya Tunduru,upungufu wa watumishi na vitendea kazi.
Naye Meneja wa Tarura wilaya ya Nyasa Thomas Kitusi,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuiongezea fedha TARURA kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo.
Joackim Kamanga mkazi wa Mbambabay anasema, kwa muda mrefu barabara katika mji wa Mbambabay zilikuwa za vumbi,hivyo kusababisha uendelezaji wa mji huo kwenda kwa kusua sua.
Anasema,ujenzi wa barabara za lami za mitaa zitawezesha mji huo kukua kwa haraka na kuvutia wageni hususani watalii wa ndani na nje ya nchi.
Sholastika Challe,amefurahishwa na hatua ya serikali kuanza kujenga barabara za lami za mitaa kwa kuwa zitachochea sana maendeleo na kukua kwa uchumi wa wananchi na wilaya ya Nyasa.