Ndege adimu duniani anayeitwa pentiole ambaye amehamia hifadhi ya Mwambesi Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma akitokea nchini Madagascar
MSITU wa Hifadhi wa Taifa wa mazingira asilia Mwambesi uliopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ulianzishwa mwaka 1956 na ulipandishwa hadhi kuwa msitu wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2017/2018.
Meneja wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Denis Mwangama katika wilaya ya Tunduru anasema msitu huo umepandishwa hadhi ili kuongeza uhifadhi zaidi kutokana na kuwa na utajiri wa viumbe vya kipekee duniani wakiwemo wanyama,ndege na mimea.
Anawataja wanyama waliopo katika msitu huo ambao upo kando kando mwa Mto Ruvuma kuwa ni simba, tembo, chuo,kuro,jamii za nyani,jamii za swala,nyati na wanyama wengine.
Mwangama anasema Katika msitu wa Mwambesi kuna jamii ya ndege maarufu duniani anayeitwa Pentiole ambaye utafiti uliofanywa na PALMS Foundation mwaka 2015 umebaini kuwa ndege huyo amehamia kutoka nchini Madagaska baada ya mazingira aliyokuwa anaishi kuharibiwa na shughuli za kibinadamu.
Kwa mujibu wa Mwangama, ndege huyo ana tabia ya kuzamia samaki kutoka majini na kwamba ndege hao wanapenda kuishi kwenye maporomoko ya Mto Ruvuma yanayoitwa Sunda ambayo yapo ndani ya hifadhi hiyo.
“Tanzania tuna bahati katika msitu wetu tuna ndege Pentiole ambaye amekuwa akiishi ukingoni mwa maporomoko ya maji yajulikanayo kama Sunda Water falls’’,anasisitiza.
Kwa mujibu wa Mwangama Ndege huyu huogolea kulingana na mawimbi ya maji yadondokayo kwenye maporomoko hayo akitatafuta mawindo yake ya samaki maana ndicho chakula chake pekee.
Licha ya ndege huyo Mwangama anayataja maporomoko ya Sunda kuwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii katika hifadhi ya Mwambesi na kwamba maporomoko hayo yalitumika wakati wa vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 ili kujificha kwenye mapango kwa juu.
Mto huu ndio uliokuwa ukitumika kwenye vita vya Majimaji ambapo watu wa makabila ya Ukanda wa Kusini hususani Wangoni walitumia maji yake katika kuzimia silaha za moto chini ya uongozi wa Kinjeketile Ngwale.
Pia eneo hilo linaaminika Wajerumani walitumia kama njia kubwa wakitokea Msumbiji katika biashara ya meno ya Tembo na Waarabu walipita pembezoni mwa mto huo kuwapitishia watumwa.
Hata hivyo anasema awali kabla ya serikali kuamua msitu huo kuwa Msitu wa hifadhi,kulikuwa na vitalu vya uwindaji wa kitalii ambapo ndani ya msitu kulikuwa na kambi ya wawindaji iliyoitwa Big Game ambayo ilikuwa na Kampuni ya uwindaji iliyoitwa Tandara Hunting Safaris.
Kulingana na Meneja huyo,msitu huo una ukubwa wa zaidi ya hekta 112,000 na kwamba umbali toka Tunduru mjini hadi ofisi za msitu huo ni kilometa 90.
“Msitu huu upo kando kando mwa Mto Ruvuma ambao pia unafanya mpaka wa asili kwa upande wa kusini magharibi mwa msitu,kupitia mto Ruvuma kuna fukwe nzuri ambazo ni kivutio kwa wageni wanapotembelea msitu huu ’’,anasema.
Meneja huyo wa TFS anasema Hifadhi ya Mwambesi pia ina wanyama wa mtoni kama mamba na viboko ambapo wakati wa masika wanakuwa wengi na kuvutia wageni wanaobahatika kutembelea msitu huo.
Anasema mtalii akiwa katika msitu wa Mwambesi anaweza kufanya utalii wa kuteleza kwenye mitumbwi katika Mto Ruvuma.
Deborah Mwakanosya ni Meneja wa Msitu wa Hifadhi ya Taifa wa Mazingira Asilia Mwambesi anasema Mwambesi ni msitu wa asili wa pili kwa ukubwa kwa Tanzania ukiongozwa na msitu wa Kilombero mkoani Morogoro.
Anasema msitu huo ambao umezungukwa na Mto Ruvuma, umesheheni baianowai mbalimbali za mimea adimu duniani ikiwemo miti aina ya mipozipozi ambayo ina tabia ya kudondosha maji,miti hiyo inapatikana sehemu chache duniani ukiwemo msitu wa Mwambesi.