Na, WAF – DODOMA
Tanzania imekuwa nchi ya tatu kwa ubora wa Huduma za maabara kati ya nchi 56 za Bara la Afrika kupata ithabati ya ubora.
Hayo yameelezwa Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, leo Mei 24, 2024Jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa vyeti kwa maabara zilizopata idhibati ya Kimataifa.
“Tuna kila sababu ya kujipongeza hili ni jambo kubwa, nawapongeza mmefanya jambo kubwa sisi kama Serikali tunajivunia ninyi wataalamu wa maabara,” amesema Dkt. Mollel
Amesema anaamini mwakani watakuwa nafasi ya kwanza, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amezidi kutoa fedha katika sekta ya afya ili wananchi waweze kupata Huduma bora na za wakika.
Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha watu wa maabara wanaendelea kuwa na maslahi na kuwataka wataalamu hao kujiamini na kufanya vizuri zaidi katika kutoa Huduma bora za maabara.
“Natoa rai kwa wasimamizi wa Hospitali kuhakikisha wanawawezesha watu wa maabara, naombeni mnaofanya maamuzi kwenye eneo la maabara hili liangalieni hawa ni watu muhimu sana katika hospitali zetu nchini.
Aidha amewatia moyo wataalamu hao na kuwambia wasibweteke kwani Serikali chini ya Uongozi wa Rais Samia umewekeza vifaa na miundombinu ya kisasa ili mwananchi aweze kupata Huduma bora za afya.
Vile vile Dkt. Mollel ameagiza vituo vya afya kutumia miongozo katika kuboresha huduma za maabara na serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia afua za uboreshaji wa huduma za afya nchini.
“Hivyo nitoe rai kwa viongozi wote tuweze kusimamia kikamilifu vituo ili vitumie miongozo yote iliyotolewa na Wizara ya Afya katika kuboresha huduma zetu za Maabara nchini kwa ubora wenye kiwango cha kimataifa,”amesisitiza Dkt. Mollel.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ubora na Uchunguzi wa Magonjwa na Matengenezo ya vifaa tiba, Dkt. Alex Magesa amesema lengo la Mkutano huo ni kutoa tuzo na vyeti kwa maabara zilizopata ithibati za kimataifa kwa mwaka wa fedha 2023-2024.
Dkt. Magesa amesema wadau wa maabara wanashirikana katika kuboresha sekta ya maabara lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora na nzuri zinatolewa ambapo kwenye kuboresha huduma wamekuwa bega kwa bega na kutatua changamoto za wataalamu wa maabara nchini.
Ametaja mafanikio yaliyopatikana mpaka Sasa ni pamoja na kujenga uwezo wa Maabara ya Taifa na kuweza kugundua magonjwa ya milipuko kama kule Kagera.
“Maabara ya Taifa imekuwa kituo cha Kanda na haya ni mafanikio makubwa kwetu”, amesema Dkt. Magesa.
Amesema mpaka sawa wamefanikiwa kufikia maabara 83 ambazo zimepata idhibati ya Kimataifa ambapo Hali hiyo inaifanya Tanzania kuwa Nchi ya 3 yenye ithibati nyingi.
Amesema kupata kupata Ithibati ni gharama kubwa hivyo wanaishukuru Serikali kwa kuweza kulisimamia uwekezaji katika upande wa maabara.