Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kikao cha mwaka kilichowakutanisha wana hisa na Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Ishmael Kasekwa akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kikao cha mwaka kilichowakutanisha wana hisa na Watendaji wa TADB.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Frank Nyabundege akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kikao cha mwaka kilichowakutanisha wana hisa na Watendaji wa TADB.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kufanikiwa kupata faida ya shilingi bilioni 14 pamoja na kutoa gawio kwa Serikali shilingi milioni 850 kwa mwaka huu, tofaui na mwaka wa jana kwani walipata faida ya bilioni 11.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24, 2024 jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kikao cha mwaka kilichowakutanisha wana hisa na TADB, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, amesema kuwa kutokana na utendaji bora wa TADB mwaka ujao wa fedha serikali inatarajia kuwaongezea mtaji wa zaidi ya bilioni 100.
Mchechu amesema kuwa gawio ambalo serikali imepata itaenda kusaidia utekelezaji wa huduma mbalimbali, huku akieleza kuwa wataendelea kufanya uwekezaji kama wana hisa katika benki ya TADB ambapo mpaka sasa kuna mtaji wa shilingi bilioni 315.
“Tunaishukuru Menejimeni ya TADB pamoja na bodi kwa kuendelea kusimamia na kuhakikisha uwekezaji wa serikali unaendelea kuimarika na kuwafikia watu wengi” amesema Mchechu.
Amesema kuwa TADB ni benki ya kimkakati, huku akieleza kuwa kwa asilimia kubwa kilimo kimeajiri watu wengi na kukuza uchumi wa Taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Ishmael Kusekwa, amehaidi kuendelea kufanya vizuri katika utendaji pamoja na kutimiza majukumu ya benki kama serikali ilivyokusudia.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Frank Nyabundege, amesema kuwa benki imeendelea kufanya vizuri na kukua kila mwaka katika utendaji wa kazi, huku akitoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa ya kupata mkopo kwa ajili ya kilimo cha mazao, ufugaji pamoja na uvuvi.
“Serikali yetu imekuwa ikitusaidia mtaji na mwaka huu imetupatia bilioni 170, tumeendelea kukua na kuwafikia watanzania wengi hasa wakulima, wafugaji na wavuvi na kufikia malengo kwa asilimia kubwa” amesema Nyabundege.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ni benki inayomilikiwa na Serikali ikiwa na lengo kuchangiza shughuli za maendeleo katika sekta ya kilimo nchini.