Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa namna linavyofanya kazi na kuhakikisha amani na utulivu inatawala.
Mtanda ametoa kauli hiyo leo Mei 24,2024 Jijini Mwanza wakati wa hafla ya kuwavisha Nishani Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika uwanja wa Polisi Mabatini.
Akiwavisha Nishani hizo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura amemshukuru Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali za kulinda raia na mali zao.
“Jambo hili, Rais Samia ameandika alama kwenye mioyo yetu kwa waliotunukiwa na wengine, ni alama ambayo inaendelea kukaa ndani ya mioyo yetu kwa muda mrefu sana” amesema IGP Wambura
Aidha, IGP Wambura amesema Jeshi la Polisi nchini limedhamilia kuhakikisha amani inatawala, uhalifu na wahalifu havina nafasi ndani ya nchi yetu.
“Hatutarudi nyuma na kuacha wahalifu wanatamba ndani ya nchi yetu” amesisitiza IGP Wambura
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Naibu kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa kwa niaba ya makamanda wa Polisi kanda ya ziwa amesema nishani zilizotolewa na Mhe Rais zimeongeza morali na uwajibikaji kwa kwenda kusimamia misingi itakayoleta mafanikio.
Hata hivyo, IGP Wambura amewakumbusha maafisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kuendelea kutekeleza mapendekezo ya tume ya haki jinai kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja.
Nishani hizo walipewa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo jumla ya maafisa 22 wakaguzi 5 na askari wa vyeo mbalimbali 5 wa kanda ya ziwa wamepewa Nishani hizo.
Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza