Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi pikipiki kwa taasisi tatu ikiwemo Jeshi la Zima moto Tanzania, The Angeline Foundation na Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) ili kuzirahisishia utendaji kazi wake.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika ukumbi wa SIWA kata ya Kirumba Mhe Dkt Angeline Mabula amezitaka taasisi hizo kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa madhumuni yaliyokusudiwa huku akisema kuwa tendo alilolifanya ni utekelezaji wa maombi yaliyowasilishwa na taasisi hizo katika ofisi yake kutaka kurahisishiwa usafiri wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za kila siku
‘.. Tunatakiwa kuwa karibu na askari wetu, iwe askari jeshi, askari polisi au zimamoto, Tunaamini kupitia pikipiki hizi kutaongeza ukaribu nao kwani wataweza kufika katika maeneo yetu Kwa wakati, kutoa elimu, kufanya kaguzi mbalimbali ikiwemo za majengo yetu ili ajali za moto zisitudhuru ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula mbali na kumshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo fedha za ujenzi wa kipande cha kilomita 10 cha barabara ya kutoka uwanja wa ndege kuelekea Kayenze mkataba wake uliosainiwa jana katika ofisi za wakala wa barabara mkoani Mwanza TANROADS amesisitiza makundi katika jamii kuhakikisha wanashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa na kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura sanjari na kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mwalimu Hasan Elias Masala kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo zinazoletwa wilayani kwake .
Kwa upande wake Mkuu wa jeshi la zimamoto wilaya ya Ilemela Afande Deusdedith Rutta amesema kuwa kwa niaba ya kamishina mkuu jenerali wa jeshi la zimamoto amemshukuru Mbunge huyo kwa kutoa pikipiki itakayowasaidia katika usafiri wa utekelezaji wa shughuli za Kila siku za jeshi hilo na kwamba hivi karibu Amir Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan ametoa magari 12 ya kisasa nchi nzima kwaajili ya kuzima moto ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi sura ya 5 inayoitaka Serikali kulijengea uwezo jeshi hilo katika kufanya kazi kwa weredi na usasa kwa kulipa vifaa vinavyoenda na wakati
Nae mwakilishi wa Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Chiguma Elias akafafanua kuwa kazi kubwa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo imefanywa ndani ya Jimbo la Ilemela na kwamba chama chake kinampongeza muwakilishi wa wananchi wa Jimbo hilo kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na kusisitiza wanachama na wananchi kuwaunga mkono Rais Dkt Samia katika nafasi ya Urais na ubunge kwa Dkt Angeline Mabula
Akihitimisha Bi Zuhura Mohamed Salaam ambae ni mwenyekiti wa SMAUJATA wilaya ya Ilemela mbali na kumshukuru Mbunge huyo kwa kukabidhi taasisi yake pikipiki akawataka wanachama wenzake kuendelea kupinga vitendo vya kikatili pamoja na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kujihusisha vitendo hivyo katika jamii