Na Ashrack Miraji Fullshagwe Media
Leo Alhamisi Mei 23,2024, Diwani wa Kata ya Njoro, Omar Abeid, alikabidhi madawati na meza kwa uongozi wa Shule ya Sekondari Mighara. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusoma, salama na rafiki wakati wote wanapokuwa shuleni.
Mhe. Diwani aliwasihi walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatunza vifaa hivyo ili viweze kutumika vizuri. Fedha za kununua madawati na meza hizi zilitoka kwenye mfuko wa Jimbo la Same Magharibi, ambazo Mhe. Mbunge David Mathayo aliwasilisha kwa wanafunzi.
Pamoja na hayo, aliwataka wanafunzi kuwaombea viongozi wa taifa, hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mhe. Mbunge David Mathayo, ili waweze kutimiza ndoto za elimu.
Mhe. Diwani alisisitiza umuhimu wa kushukuru viongozi hao kwa kazi nzuri wanazofanya kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Same Magharibi wanapata huduma stahiki.
Khadija Said, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, alitoa pongezi kwa Mhe. Mbunge David Mathayo kwa kuboresha mazingira ya kusoma. Kabla ya hapo, walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosa viti na meza bora. Sasa wanaweza kusoma kwa utulivu na wanamuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga madarasa zaidi nchini kote. Hii ni ishara ya uzalendo wa kweli!