Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda , ameonesha hali ya kushangazwa na kuchukizwa mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa kisima cha maji uliopo kijiji cha Ilidonyo Kata ya Sinya katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido uliotumia kiasi cha fedha takribani Tsh Milioni 600 na bado wananchi hawajanufaika kwa kupata maji kutokana na mradi huo.
RC Makonda amefika na kutembelea katika mradi huo katika muendelezo wa ziara yake aliyoipa jina la SIKU 6 ZA MOTO ARUSHA ambapo ameanzia leo katika Wilaya ya Longido.
Akikagua mradi huo, RC Makonda amehoji kuhusiana na package ya Tsh Bilioni 520 ya mradi wa maji uliohusisha uchimbaji wa visima 56 ambapo kimoja wapo ndicho cha Longido, kwanini hakijawekewa usanifu wa mtandao wa usambazaji maji kwa wakazi wa eneo hilo.
Katika majibu, AUWSA wamesema bajeti iliyokuwepo ni ya kusambaza maji kupeleka maeneo mbalimbali katika Jiji la Arusha pekee.
Kulingana na majibu hayo, RC Makonda alihoji kutaka kujua ni umbali gani umetumika kusambaza maji Arusha Jiji na kushindwa kusambaza maeneo ya Namanga ambapo ni umbali wa Kilomita 35 pekee pamoja na maeneo ya Longido ambapo ndipo kisima kimojawapo kilipo na ni umbali wa Kilomita 1.9 pekee ili kusambaza maji kwa wananchi.
Katika majibu yake , Kaimu Mkurugenzi wa AUWSA Mhandisi. Upendo Shushu , amekiri kuwa kwasasa kisima hicho hakiwanufaishi wakazi wa Longido.
Kulingana na majibu hayo, RC Makonda ameonesha wazi kusikitishwa kwakuwa katika mradi huo mkubwa wa Tsh Bilioni 520 kulikuwa na mtandao wa usambazaji maji wa kilomita 900 ndani yake lakini cha kusikitisha na kushangaza ni kuona sehemu mojawapo ambapo kisima kimechimbwa (Longido) wakazi hawanufaiki na kisima hiko angali mtandao wa kuwasambazia maji ni kilomita 1.9 pekee.