Handeni, Tanga
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za Kijamii na kiuchumi (RISE) unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ipo kwenye hatua za usanifu wa barabara za awamu ya pili zenye jumla ya Km. 164 katika Mikoa ya Tanga, Geita na Lindi.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga, Mhandisi George Tarimo amesema mradi huo wa RISE unatarajia kujenga barabara za lami zenye jumla jumla ya Km. 107 katika Wilaya ya Handeni Kufikia mwaka 2026 ambapo Km. 57 tayari Mhandisi Mshauri yupo ‘site’ anaendelea na kazi za usanifu.
Amesema barabara zinazofanyiwa usanifu kwa sasa ni Sindeni-Kwedikwazu Km. 38 na Michungwani-Bondo-Kwadoya Km. 19.
Ameongeza kuwa awamu zinazofuata zitajengwa barabara ya Mkata-Kwasunga Km. 22, Kwachaga-Kwankonje Km. 10 na Mzundu-Kabuku Km. 18.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Albert Msando ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa suluhisho kwa wananchi wa Wilaya hiyo ambao ni wakulima wa matunda na mbogamboga kwani kwa sasa wanatumia gharama kubwa kusafirisha machungwa kutokana na hali ya barabara kuwa mbaya.
Pia Mhe. Msando amewaasa wananchi kulinda na kudumisha amani ikiwemo usalama wa Wakandarasi na Wahandisi Washauri katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo.
Aliongeza kuwa, wananchi wa Wilaya ya Handeni wanapaswa kuchangamkia fursa ya ajira zitakazopatikana kupitia mradi huu lakini pia fursa za biashara na huduma zitakazo hitajika wakati wa ujenzi.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Sindeni, Mhe. Mohamed Kilongola ameishukuru serikali kwani ameona hatua za mwanzo za kutekelezwa kwa mradi zimeanza na wananchi wanashirikishwa katika kila hatua ikiwemo kushiriki vikao kuhusu mradi huo na wamepatiwa elimu kuhusu masuala ya kijamii na fursa za kiuchumi zitakazopatikana kipindi cha utekelezaji wa mradi huo.
Wakiongea kwa wakati tofauti wakazi wa vijiji vinavyopita mradi huo Bw. Bakari Omari mkazi wa kijiji cha Kwamdudu ameishukuru serikali kwa kuweka barabara yao kwenye mpango wa kuwekewa lami kwani barabara hiyo itakapo kamilika itawarahisishia kusafirisha mazao yao kwa urahisi sokoni lakini pia daraja la mto msangazi likijengwa litasaidia kuunganisha kata ya Ndolwa na karibu vijiji nane kwenda hospitali ya Kwamkono.
Pia Bi. Mary Raphael mkazi wa Kijiji cha Komfungo alisema barabara hiyo ikijengwa itaunganisha Kata ya Sindeni, Ndolwa, Komkonga na Kabuku na kuwasaidia wananchi wa huko kufanya biashara kwa mafanikio makubwa na kuongeza uchumi wao.