Baada ya benki ya wananchi Njombe NJOCOBA kuingia mufilisi mwaka 2018 na kisha fedha za wateja 8309 kati ya wateja 12,323 kushikiliwa kwa miaka kadhaa na kisha kusababisha malalamiko na mashaka kwa wakazi wa Njombe,Hatimae maofisa na wataalamu kutoka Bodi ya amana nchini DIB wamelazimika kupita kwenye maeneo ya mikusanyiko yakiwemo Masoko na Vituo vya mabasi kutoa elimu ya amana na kisha kuwataka wateja wote wanaoidai benki hiyo kwenda kuchukua fedha zao.
Wakiwa katika soko la Wakulima lililopo kando ya jengo la NJOCOBA kwa lengo la kutoa elimu ya amana wafanyabiashara na wateja wa taasisi za fedha maofisa wa DIB wakiongozwa na Joyce Shala ambaye ni ofisa rasilimali watu wamesema hakuna mtu atakaepoteza haki zake hivyo anatoa rai kwa wateja kutoka matawi ya wilaya ya Ludewa,Makete na maeneo mengine kwenda kuchukua fidia ya amana zao huku Denis Mrema akisema licha ya kulipa bil 1.28 lakini bodi inawatafuta watu 2287 wanaodaiwa mil 431 na njocoba
“Nitoe rai kwa watu wote wanaodai fedha zao Njocoba wafike mara moja benki ya TCB walipe haki zao na wale ambao wanadaiwa walipe ila zoezi la DIB likamilike na kuendelea na kazi nyingine,alisema Denis Mrema kutoka kitengo cha uhasibu” .
Kitendo cha maofisa wa DIB kukutana na watendaji wote mitaa na vijiji na kisha kupita katika maeneo ya mikusanyiko mkoani Njombe kutoa elimu kuhusu amana na taarifa za ulipaji wa fidia zilizoshikiliwa NJOCOBA kwa zaidi ya miaka 6 kunawaibua wanufaika akiwemo Edward Godiwe ambao wanasema matumani yaliyokufa yamerejea.
“Kwa kweli kipindi chote benki imefungwa nilipoteza imani ya kupata fedha yangu zaidi ya mil 6 zilizokuwa nimeweka benki ya NJOCOBA lakini imani imerejea baada ya maofisa wa bodi hii kuja kutupa elimu na kukiri kuanza kutulipa haki zetu hizi,milioni sita sio ndogo kwangu,alisema Edward Godiwe”.
Nao baadhi ya wafanyabiashara waliopatiwa elimu ya amana na biashara kutoka soko la wakulima mjini Njombe na soko kuu wamesema kulipwa kwa waliokuwa wakidai NJOCOBA kutarejesha imani kwao kuanza tena kuweka fedha benki.