Waziri wa Madini Anthony Mavunde akifungua jukwaa hilo mkoani Arusha leo .
……..
Happy Lazaro,Arusha .
Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameitaka Tume ya madini nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote katika utoaji wa mikataba kwa kuhakikisha wanatangaza zabuni ili haki iweze kutendeka.
Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo leo mkoani Arusha wakati alipokuwa akifungua jukwaa la tatu la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya Madini linalofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Aicc jijini Arusha.
Aidha amesema kuwa ,kumekuwepo na miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakitoa mikataba bila kutangaza zabuni jambo ambalo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na jambo hilo halitakiwi kufumbiwa macho kabisa .
“Nawaomba sana msitoe mikataba bila kutangaza zabuni ili haki iweze kutendeka hivyo hakikisheni mnaboresha eneo hilo ili watanzania waweze kunufaika pia kwani tunataka kipaumbele kwanza kwa watanzania .”amesema Mavunde .
Aidha amewataka watanzania kujenga utaratibu wa kusaidiana wasiwe na wivu katika utendaji kazi wao kwani kwa kufanya hivyo hawawezi kufanikiwa kamwe badala yake wajenge utaratibu mzuri wa kusaidiana .
Aidha Mavunde ameongeza kuwa,sekta ya madini hapa nchini imefanikiwa kuongeza ukuaji wa pato la taifa kutoka asilimia 5.1 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 9.1 mwaka 2023.
Ameongeza kuwa ,kutokana na mafanikio hayo serikali imeongeza bajeti katika sekta ya madini kutoka sh,bilioni 89 hadi sh,bilioni 231 na fedha hizo zimeelekezwa kwenye utafiti zaidi wa madini na kuboresha maabara kwa lengo la kukuza sekta hiyo.
“Katika mwaka wa fedha 2024/25 unaoanza Januari mtashuhudia ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa mjini Dodoma na mchakato wa ununuzi wa helkopta kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina wa madini kwani hadi sasa utafiti umefanyika kwa asilimia 16 na lengo ni kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030″amesema Mavunde.
Hata hivyo amesema sera ya madini ya mwaka 2009 ilisababisha malalamiko mengi kwa watanzania juu ya ugumu wa kushiriki moja kwa moja katika sekta ya madini.
“Pamoja na uwepo wa sera ya madini ya mwaka 2009 ,serikali iliona ipo haja ya kuifanyia mabadiliko sheria ya madini ya mwaka 2010 na ilipofika mwaka 2017 serikali ilifanya mabadiliko iliyoendana na utungwaji wa kanuni na hivyo kuwapa fursa watanzania kushiriki kwa wingi katika uwekezaji katika sekta hiyo na kunufaika na rasilimali hiyo “
Amesema wizara ya madini inatekeleza mtazamo wa kufikia asilimia 50 ya utafiti wa eneo la madini nchi nzima ifikapo 2030.
“Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yametoa fursa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini”Alisema Mavunde na kuongez kuwa
Marekebisho ya mwaka 2017 ya Sheria ya Madini, yalipelekea kutungwa kwa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini,”
Katika hatua nyingine Waziri Mavunde amesema mwaka wa fedha uliopita 2022/23 serikali ilifanikiwa kukusanya maduhuli ya sh,bilioni 678 baada ya kufanyika biashara ya madini yenye thamani ya sh, trilioni 1.7 katika vituo 100 vya manunuzi na masoko 42 na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni zaidi ya asilimia 56 .