Benki ya NMB imesema inaipa sekta ya kilimo jicho la pekee kwa kuhudumia katika mnyonyoro mzima kuanzia mkulima mwenyewe kwa kuwapa mikopo ya riba nzuri kwa asilimia tisa ili waweze kufanya kilimo chenye tija na cha kisasa.
Hatua hiyo imeelezwa na Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola wakati mkutano wa wafanyabiashara na benki hiyo (bussines club) kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe.
“Tunahudumia sekta ya kilimo kuanzia mnyororo wake mzima kwa maana yake kuanzia mkulima anayelima shambani, mtu anyeuza mbolea, msambaza mbolea mtu anayeuza mazao, madawa yani mnyororo mzima wa kilimo sisi tunafanya nao kazi kwae hiyo tunawapa mikopo kulingana na shughuli anayofanya,” amesema.
Amesema wanafanya mikutano hiyo mara kwa mara ili kuwakutanisha wateja ambao ni wa kilimo na wafanyabiashara kwa pamoja ili kuweza kueleza fursa zinazopatikana kwenye benki hiyo.
“Ni jukwaa ambalo wanapata mengi yanayohusu, yanayotokea tangu tumeanza na kukutana mara ya mwisho na wao na sisi NMB kuna mabadiliko makubwa yametokea huku ndani na tunatumia hii fursa kuwajulisha,” amesema Chilongola.
Chilongola amesema benki ya NMB inafanyia kazi changamoto za wateja ili kuhakikisha wanasonga mbele.
“Lakini pia tunawapa fursa ya kujifunza kwa sababu kuna maafisa wa serikali, ofisa ardhi, ofisa leseni na ofisa biashara wanatoa elimu pia kwa wateja na wenyewe ni jukwaa la kukutana na kubadlisha mawazo na kufanya mtandao kwa ajili ya kushirikiana katika biashara zao,” alisema Chilongola.
Meneja Mwandamizi kutoka NMB kitengo cha biashara, Christopher Mgani ameema hivi sasa benki hiyo imewateletea wafanyabiashara na wakulima mikopo ambayo inachangia kwenye suala zima la vifaa kazi.
“Vifaa kazi ni vitu ambavyo biashara inahitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli zake mbalimbali, ikiwemo vifaa vya kutembea na visivyohamishika na tunavileta kwa sababu tunaamini changamoto kubwa ya wafanyabiashara ni suala la dhamana lakini ukichukuwa mkopo wa kifaa tunafanya kifaa hicho hicho kuwa ndiyo dhamana yako,” amesema Mgani.
Mmoja wa wafanyabiashara Edna Shakazulu amesema anaishukuru NMB kwa kuwawezesha wafanyabiashara kwa kuwakopesha fedha kwa wakati na kuomba kuondolewa kwa changamoto kuchelewa kurudi kwa taarifa za mikopo mikubwa kutoka makao makuu.