Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amewavalisha Nishani Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Mikoa ya Kanda ya kaskazini ikihusisha Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Shule ya Polisi Moshi Mkoani Kilimanjaro Mei 22,2024.
Nishani hizo walipewa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Ambapo jumla ya maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali 630 wametunikiwa nishani ikiwemo Nishani ya kumbukumbu ya Mungano, Nishani ya Utumishi uliotukuka, Nishani ya Utumishi wa Muda mrefu, Nishani ya utumishi Mrefu na Tabia Njema.
……….
Mchungaji Benjamin Bukuku wa kanisa la TAG amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini hususani Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo linaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya vitendo vya uhalifu pamoja na umuhimu wa kutunza amani ya taifa.
Mchungaji Bukuku ameyasema hayo wakati wa hafla ya uvishaji wa nishani iliyofanyika katika shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kutoka Kanda ya Kaskazini inayohusisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Kwa upande wake kiongozi wa kanisa Katoliki lililopo katika Shule ya Polisi Moshi Padri Daniel Amani amewapongeza waliotunukiwa nishani na kuwaasa waende wakatimize majukumu yao kwa misingi ya sheria na kutii maagizo yanayotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amewataka Makamanda wa Polisi pamoja na askari waliotunukiwa nishani hizo Kwenda kufanya kazi kwa kuzidisha tija na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao na kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma bora na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Naye mkuu wa Shuke ya Polisi Moshi SACP Ramadhani Mungi akiwawakilisha wenzie aliotunukiwa nao nishani na Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa niaba ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amesema watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa nidhamu, weledi na uadilifu na kutoa huduma bora kwa wananchi