Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuitafsiri kwa vitendo kaulimbiu yake ya “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu” ambapo wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wameendesha mafunzo ya kuhusu uadilifu katika jamii kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mount Calvary iliyopo Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanafunzi wa darasa la awali hadi darasa la saba pamoja na walimu wa shule hiyo yameangazia eneo la uadilifu katika jamii kama nyanja kuu inayopaswa kupewa msisitizo zaidi ili kuiweka Tanzania ya kesho katika mikono salama.
Akiongea kwa niaba ya wahadhiri walioshiriki katika kutoa mafunzo hayo, Mhadhiri Msaidizi Joseph Masaga akiongozwa na kauli mbiu ” Tanzania salama ipo mikononi mwa Watanzania wenyewe.” ametoa msisitizo kwa walengwa kwamba ni jukumu la kila mwanajamii kuifanya jamii na Tanzania kiujumla iwe sehemu salama ya kuishi kwa kila mmoja wetu.
Mhadhiri Masaga amesema kuwa ni muhimu kwa watoto na vijana kujikita katika utu na uwajibikaji ili kutambua umuhimu wa vijana katika taifa la kesho na kuwaasa kutojihusisha na vitendo vinavyokiuka miiko na maadili katika jamii zao.
Ameongeza kuwa mara kwa mara tunasikia taarifa za watoto na vijana wamekuwa kufanyiwa vitendo vya ukatili kitu ambacho ni kinyume na mila na desturi za taifa letu hivyo hatuna budi kuwalinda watoto na vijana katika hili wimbi ili kuweza kulinda utu wao kwa kuwafundisha kujua utu wao, uadilifu na kuwajibikaji.
“Vijana wanapoishi katika jamii zao wanapaswa kuhakikisha kwamba wanafuata misingi bora wanayoelekezwa na wakubwa zao katika kuyaishi maisha yao huku wakiwa wanajiandaa na majukumu yao ya huko mbeleni. Alisisitiza Mhadhiri Masaga.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Mount Calvary Bi. Esther Gama ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam katika kuhakikisha elimu ya uadilifu katika jamii inawafikia vijana na kuongeza kwamba uadilifu katika jamii ni chachu ya maendeleo.
Bi. Gama kwa niaba ya menejimenti ya Shule hiyo ameupongeza uongozi wa Ndaki ya Dar es Salaam kwa jitihada wanazozionesha katika kuelimisha jamii na kusisitiza mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana ili waweze kutambua utu wao wangali bado wadogo.
Chuo Kikuu Mzumbe katika kutekeleza mpango mkakati wa chuo ikiwemo kurudisha huduma kwa jamii , kimekua kikitoa misaada na huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo misaada ya kijamii, mafunzo mbalimbali kwa jamii pamoja na msaada wa kisheria bure kwa jamii.