Mgombea nafasi ya uenyekiti Kanda ya Victoria John Pambalu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
………..,……………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kuelekea uchaguzi wa kuwachagua viongozi mbalimbali wa Kanda ya Victoria utakao fanyika Mei 25, 2024 John Pambalu mgombea nafasi ya uenyekiti wa Kanda hiyo ameeleza vipaumbele vyake atakavyo vifanya pindi atakapochaguliwa.
Vipaumbele hivyo amevitaja leo Mei 20, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Middlend Jijini Mwanza.
Pambalu amesema atahakikisha anawatambua watia nia wa Ubunge,Udiwani pamoja na Mtaa wanaotaka kuwa viongozi kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili wawape majukumu ya kufanya hatua itakayosaidia kupata ushindi kwenye vitongoji na vijiji vingi.
“Nitahakikisha tunawatambua wagombea wa vijiji na vitongoji kabla ya mwezi wa 6 mwaka huu ili waweze kupewa mafunzo kabla ya uchaguzi”, amesema Pambalu
Aidha, ameeleza kuwa atahakikisha nidhamu ndani ya chama kwani hakuna Jeshi lililowahi kufanikiwa bila kuwa na nidhamu huku akiongeza kuwa nidhamu ni pamoja na kuwaheshimu watu walioko chini ya madaraka.
“Nikichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria nitahakikisha Kanda yangu haina migogoro,pia nataka Kanda nitakayoiongoza ibuni oparesheni zake yenyewe na kusimamia bila kusubili Taifa kuleta oparesheni,Mfano Kagera nafikiria kuanzisha oparesheni inayoitwa IMUKA”, amesema Pambalu
Pambalu amesema ahadi yake kwa wana Victoria ni MUNOFU ambapo M ni mafunzo,U ni ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu,N ni nidhamu na umoja O ni oparesheni za kisiasa hasa vijijini F ni fursa sawa kwa wote na U ni ujenzi wa Ofisi.
Mwisho Pambalu amesema anaamini katika mafunzo kwa sababu Chama chake kimemfundisha hadi akawa Mwenyekiti wa Baraza la vijana Taifa.