…………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.MAWAKILI wa serikali nchini wametakiwa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma,nidhamu,uzalendo,
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ,Jumanne Abdallah Sagini wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa serikali mkoani Arusha .
Sagini amesema kuwa ili utumishi wao uwe wenye ufanisi na kuheshimika wanapaswa kuzifuata kanuni za maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na tabia na mienendo inayozingatia utoaji wa huduma bora,utii kwa serikali ,utoaji wa huduma bila upendeleo pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu ,kuwajibika kwa umma.
Aidha amesema kuwa ,mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali ambapo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili wa serikali katika kusimamia mashauri ya madai na usuluhishi kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili stahiki.
Ameongeza kuwa ,katika mafunzo hayo watafundishwa mada kuhusu masuala ya usimamizi na utatuzi wa migogoro inayotokana na sekta ya ujenzi,na utatuzi wa migogoro inayotokana na mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa migogoro itakayotokea kwenye uwekezaji inashughulikiwa kwa haraka na kwa gharama nafuu na kulinda mahusiano ya kibiashara kati ya wawekezaji na serikali.
“Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni uungaji mkono juhudi za Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya “Mama Samia Legal Aid “ambayo lengo lake kuu ni kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wote hapa nchini pamoja na sera ya kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini,kwani kupitia ujio wa wawekezaji serikali itaingia mikataba mbalimbali ambayo itahitaji kupata ushauri na majadiliano wakati wa kuingia na pale tofauti zinapokuwa zimejitokeza kati ya serikali na wawekezaji. “amesema Sagini.
Kwa upande wake Wakili Mkuu wa serikali ,Dk Boniphace Nalija Luhende amesema kuwa,amesema mafunzo hayo yanajumuisha mambo matatu ikiwemo uzinduzi wa nembo ya ofisi ya Wakili mkuu wa serikali ambayo itatambuliwa kama OWMS,ambapo mafunzo hayo yanahusu uwasilishaji wa mada mbalimbali pamoja na majadiliano kwa muda wa siku tatu za mafunzo hayo ,pamoja na kupata muda wa kujitathimini namna ambavyo wametekeleza majukumu yao na kuendesha na uratibu mashauri ya madai na usuluhishi.
Luhende ameongeza kuwa,OWMS imekuwa na desturi ya kutoa mafunzo kwa mawakili wa serikali kila mwaka kwa lengo la kuongeza maarifa na ujuzi zaidi katika maeneo mtambuka ambayo mawakili hujishughulisha nayo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa weledi mkubwa zaidi.
Ameongeza kuwa ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ,OWMS inahitaji kuwa na mawakili wenye uelewa na uwezo mkubwa katika uendeshaji wa mashauri mbalimbali ya serikali na mafunzo ya mwaka 2024 yamekuja na kauli mbiu ya “Uendeshaji wa mashauri ya serikali, :Wajibu na majukumu ya Wakili wa serikali”.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa serikali,Alice Mtulo amesema kuwa ,mafunzo hayo ni mwendelezo wa mipango ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali pamoja na Mawakili wa serikali waliopewa hati idhini ya kuendesha mashauri kwa niaba ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali .
Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanajumuisha washiriki kutoka katika wizara,Taasisi,Mashirika ya Umma,Mamlaka za Serikali,Serikali za Mitaa,Tume mbalimbali za Serikali na Bodi mbalimbali.