Na Khadija Khamis Maelezo. 19/05/2024.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Godfrey Eliyakimu Mzava amesema vijana wanashindwa kutoa mchango wa maendeleo katika taifa lao kutokana na kushiriki katika utumiaji wa dawa za kulevya.
Ameitoa kauli hiyo huko Skuli ya Sekondari ya Hassan Khamis Hafidhi wakati akizindua klabu, na kufunga mafunzo ya rushwa, kupambana na madawa ya kulevya ukatili wa kijinsia na mabadiliko ya tabia ya nchi sambamba na kugawa review za masomo ya sayansi kwa wanafunzi na kukabidhi vifaa vya maabara katika mradi wa elimu.
Amesema hali hiyo inapelekea vijana kupoteza muelekeo na nchi kukosa nguvu kazi ya taifa.
“Vijana wamekuwa wakitumia uraibu huo na kushindwa kutoa mchango katika taifa lao hata jamii, inasikitisha kuona kwamba vijana wa kutegemewa wamegeuka kuwa tegemezi kwa familia na taifa.” alisema Kiongozi huyo.
Amesema vijana ndio nguvu kazi ya taifa ambao wanategemewa kutoa mchango mkubwa wa ujenzi wa Nchi hivyo ipo haja ya jamii na serikali kukemea na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha amesema rushwa ni aduwi wa haki na inarudisha nyuma juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau wa maendeleo katika kukuza Uchumi wan chi.
Sambamba na hayo, ameisisitiza jamiii kuengeza nguvu katika uhifadhi wa mazingira, upandaji wa miti uondoshaji wa taka ngumu na kutoa elimu kwa jamii ikiwemo kwa wanafunzi ili kuweka mazingira katika hali safi na ya kuvutia.
Aidha alisisitiza kuwa vijana hao waendelee kupewa mafunzo ya rushwa,mazingira, elimu dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto ili kuweza kuwa mabalozi wazuri kwa jamii.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Simai Msaraka amesema jumla ya sh. milioni 53 zimetumika katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Wilaya ya Magharibi ‘A’ Asha Mohamed Omari amesema jumla wanafunzi 150 Skuli mbalimbali ikiwemo Mwera, Munduli na Bububu wamepatiwa mafunzo kupitia mradi wa elimu ili kupiga vita rushwa, Dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Amesema katika mradi huo wameweza kugawa review za masomo ya sayansi kwa wanafunzi na kukabidhi vifaa vya maabara ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika wilaya hiyo.
ujumbe wa mbio za mwenge mwaka 2024 ni “umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa taifa”.