Na: Dk. Reubeni Lumbagala.
Mwanafalsafa mmoja wa kiroho aliwahi kusema kwamba mtu aliyepewa dunia na muumba wake ni yule anayeamka asubuhi akiwa na vitu vitatu vifuatavyo: amani, chakula cha siku hiyo na afya. Kuhusu suala la afya ambalo makala hii linaiangazia zaidi, utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa unategemea uwepo wa vitu vingi, lakini kubwa miongoni mwa hayo ni uwepo wa wataalamu wenye ujuzi, maarifa na weledi.
Kukosekana kwa wataalamu wa kuwahudumia wagonjwa, kunapelekea vifo na matumizi makubwa ya fedha kwani wagonjwa watalazimika kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu, jambo linaloongeza gharama za matibabu kutokana na kugharamia nauli, chakula, malazi na matibabu yenyewe.
Na kumbuka hilo la kwenda nje kutafuta matibabu wanaomudu ni wachache na hivyo naweza kusema tumepoteza Watanzania wengi miaka ya nyuma kutokana na kukosa madaktari bingwa na bobezi katika nchi yetu. Gharama za kutibiwa nje mara nyingi huwa zaidi ya mara mbili kama ugonjwa uleule utatibiwa hapa nchini.
Ni ukweli uliodhahiri kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi shupavu wa Dk. Samia Suluhu Hassan umejipambanua pasi na shaka kuipa msukumo na kipaumbele sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, na kuwajengea uwezo raslimali watu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) inatoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaosomea kozi mbalimbali, ambapo miongoni mwa hizo ni wanafunzi wanaosoma kozi za afya ili kuongeza wigo wa wataalamu wa afya watakaotumia maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali katika kuwahudumia Watanzania.
Katika eneo ambalo bado hatujawa na wataalamu wa kutosha ni la ubingwa na ubingwa bobezi. Kutokana na uhaba wa wataalamu hawa, Rais Samia ameweka mkakati wa kutoa ufadhili wa masomo unaogharimu bilioni 10.9 ili Watanzania wengi waweze kusoma na hatimaye kupunguza upungufu uliopo sasa katika eneo hilo muhimu.
Fedha hizi zimetengwa ili kuwezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi kupitia mradi wa Dk. Samia Super-Specialized Scholarship Programme kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Chama Cha Madaktari Bingwa na Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHYTA) jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema: “Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa madaktari bingwa katika kuwaendeleza kitaaluma kupitia programu ambayo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024, kwa wanafunzi 1,109 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 ukilinganisha na mwaka wa masomo 2022/2023.”
Utoaji wa ufadhili wa masomo kwa madaktari bingwa na bingwa bobezi ni njia bora inayohakikisha upatikanaji wa wataalamu wa uhakika kwa manufaa ya nchi yetu badala ya kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi kuja kutoa huduma nchini kwetu ambao wanagharimu fedha nyingi kuwaleta nchini au kupeleka wagonjwa wetu nje.
Ni jambo muhimu kwa taifa kujitosheleza kwa wataalamu wake wa ndani ili kuwa na uhakika wa huduma bora za afya. Hivyo basi, uwekezaji huu mkubwa wenye lengo la kuhakikisha nchi yetu inakuwa na madaktari bingwa na bingwa bobezi ni jambo la kupongezwa sana.
Madaktari hawa wanategemewa kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya ndani kama vile shinikizo la damu, kisukari, figo, magonjwa ya watoto, mifupa, upasuaji, macho, kinywa na meno, pua na koo, upasuaji wa watoto wenye midomo sungura, masikio, ngozi, moyo, mfumo wa chakula pamoja na magonjwa ya saratani.
Wataalamu hawa watakapohitimu masomo yao, watakuwa na jukumu la kutumia elimu waliyoipata katika kuwahudumia wananchi wa maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Huduma watakazozitoa kwa wagonjwa zitasaidia sana kuokoa maisha ya wananchi kwani kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa na upungufu wa wataalamu hawa ambao ni muhimu sana kwa mustakabali wa afya na ustawi wa wananchi.
Kutokana na maboresha makubwa katika sekta ya afya, wapo wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao sasa wanafuata huduma za afya Tanzania. Kwa hiyo, uwepo wa madaktari hawa bingwa na bingwa bobezi sambamba na serikali ya Dk. Samia kuleta vifaa tiba za kisasa, kunatoa fursa kwa sekta ya afya kuongeza mapato kutokana na kupokea wagonjwa wa ndani na nje ya nchi wanaofuata huduma za afya Tanzania na hivyo kunyanyua utalii wa kimatibabu nchini mwetu.
Akizungumza wakati wageni kutoka Sierra Leone walipowasili katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge alisema: “Tumepata ugeni wa wenzetu kutoka Sierra Leone wamekuja kuona maendeleo haya kuanzia tulipoanza hadi sasa wamekuja kujifunza viongozi wetu wanavyotuongoza na kuwa na taasisi kama hii. Vilevile wamekuja kuona utendajikazi wa wahudumu wetu wa afya wanavyofanya kazi ili wanapokwenda kuanzisha taasisi kwao wawe na uelewa wa kutosha.
“Pili wamekuja kujifunza ili kuleta wagonjwa kutoka Sierra Leone kuja kutibiwa hapa kwani wamejionea wenyewe kuwa watatibiwa vizuri na hii ni sehemu ya tiba utalii ambayo Rais pia amefanya.” Ni jambo la faraja kuona Tanzania leo imekuwa shamba darasa katika sekta ya afya kwa mataifa mengine kuja kujifunza na kutibiwa. Haya yote yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema.
Katika muktadha huo, Waziri Ummy alisisitiza: madaktari wenye ubobezi katika maene mbalimbali ikiwemo wa masuala ya magonjwa ya ndani.” Kuwatambua na kuwawekea mazingira bora madaktari bingwa na bingwa bobezi ili kutoa huduma kwa wananchi ni muhimu sana kwani itawavutia kufanya kazi ndani ya nchi na katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na hivyo kuwafikia wananchi wengi kwa huduma bora za kimataifa.
Vipaumbele vya kisera vya sekta ya afya kwa mwaka 2024/2025 ni pamoja na raslimali watu. Raslimali watu ni wataalamu wa afya ambao wizara imepanga kuwajengea uwezo kwa kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili kuendana na mazingira na mahitaji ya utoaji wa huduma bora za kiafya za kisasa na zenye viwango bora.
Ikumbukwe kuwa dhamira ya Rais Samia ni kupata wataalamu bingwa na bobezi wa kutosha wa kuweza kuhudumia halmashauri zote 184 hapa nchini na ndiyo maana kila mwaka kumekuwa na ongezeko la raslimali fedha zinazotengwa kwa ajili ya kufanikisha azma hii. Mathalani kwa mwaka wa fedha 2021/2022, serikali ilitenga bilioni 3, mwaka 2022/2023 bilioni 8 na mwaka 2023/2024 bilioni 10.9 ili kusomesha madaktari bingwa na bingwa bobezi katika magonjwa mbalimbali.
Mei 6, 2024 Waziri Ummy Mwalimu alizindua Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Rais Samia Katika Hospitali za Wilaya. Uzinduzi huu ulifanyika kwenye Hospitali ya Manispaa ya Iringa (Frelimo), Iringa, huku ukichagizwa na kaulimbiu isemayo *“Tumekufikia, Karibu Tukuhudumie.”*
Kwa mujibu wa Waziri Ummy, miongoni mwa mafanikio ya wataalamu hawa ni kupunguza vifo vya watoto wachanga. “Mpango Kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia utasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuwajengea uwezo watoa watoa huduma wengine katika hospitali za halmashauri kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwa na wodi maalumu za watoto wachanga (NCU) katika hospitali hizo kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye siku 0-28.
Tunaweza kuokoa maisha ya watoto wachanga endapo tutaanzisha wodi maalumu za watoto wachanga, tukaviwekea vifaa tiba ili endapo mtoto akiwa na changamoto yoyote aweze kupata huduma,” amesisitiza Waziri Ummy. Vilevile, kwa mujibu wa Waziri Ummy, Rais Samia ameweka rekodi duniani kwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80, kutoka vifo 556 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka hadi vifo 104 kati ya 100,000.
Wakati serikali ikiendelea kusomesha watalaamu hawa ili kuongeza idadi kubwa zaidi, madaktari bingwa na bobezi waliopo sasa wanawajengea uwezo madaktari wengine katika halamshauri mbalimbali nchini huku wakitoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha huduma bora za kibingwa zinatolewa nchini na kuwafikia wananchi wote ili kupunguza gharama za kutibiwa nje ya nchi haina tone la shaka. Kwani nikisema Mama Samia hana baya kwenye sektya ya afya, nitakuwa nimekosea kwa uwekezaji na utashi mkubwa wa kisiasa aliouonyesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake?
Kongole Mama Samia kwa kuipa msukumo mkubwa sekta ya afya nchini kwa maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi. Watanzania sasa tunaamka tukiwa na uhakika pia wa afya zetu mbali na amani pamoja na chakula. Hayo mawili; chakula na amani jinsi Rais Samia anavyoyapambania kupitia mikati yake na R zake nne, nitayajidili siku nyingine panapo majaaliwa.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: 0620 800 462.