Na Sophia Kingimali.
Kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini imeipongeza serikali kupitia wizara ya nishati kwa utekelezaji wa mradi wa kituo cha kupoza umeme pamoja na mradi wa njia ya kusafirishia umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo hiko Mei 18,2024 Chalinze mkoa wa Pwani Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Kirumbe Ng’enda amesema ni kazi kubwa imefanyika katika kituo hiko ikiwa ni katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
“Tulikuja hapa mwezi wa tatu kuangalia maendeleo ya kituo hiki na kilikuwa kimefika asilimia 55 na tulipata wasisi na kuwaomba waongeze spidi kwa maana bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa kwenye spidi kubwa na leo tumejionea kutoka asilimia 55 mpka kufikia asilimia 93.5 kazi kubwa imefanyika tunawapongeza sana serikali kupitia wizara hii ya nishati”,Amesema.
Amesema kukamilika kwa mradi huu utachochea sera ya nchi ya uchumi wa viwanda kwa kuwa hakuna maendeleo ya viwanda pasipokuwa na nishati ya umeme.
Aidha ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu pia kunaenda kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme lakini pia ukizidi utaweza kuuzwa kwa nchi jirani na hivyo kuchochea uchumi wa nchi kuzidi kukua.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema miradi hiyo ambayo ipo ukingoni kukamilika ilianza mwaka 2021 chini ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Tunapomaliza miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt Samia tunayo miradi ya kujivunia njia ya kusafirishia umeme na kituo cha kupoza umeme yote ilianza 2021 ni miradi ambayo ilianza na awamu ya sita ambapo mradi wa njia ya kusafirishia umeme umefikia asilimia 99.5 na kituo cha kupoza umeme umefikia asilimia 93.7 miradi inatekelezeka na ipo mbioni kukamilika”,Amesema.
Pia ameipongeza TANESCO kwa usimamizi mzuri miradi hiyo ambayo imekuwa na tija na maslahi mapana kwa Taifa.
Akizungumzia swala la upatikanaji wa umeme nchini amesema umeme upo wa kutosha na nchi imeanza kunufaika kutokana na bwawa la Julius Nyerere ambapo megawati 235 za mashine namba 9 kutoka bwawa la JNHPP zinapitishwa kwenda kwenye kituo cha kupoza umeme Chalinze.
Amesema ukatikaji wa umeme kwenye baadhi ya maeneo hausababishi na ukosefu wa nishati hiyo bali unatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirishia umeme.
“Miundombinu kwenye baadhi ya maeneo ni chakavu na ya siku nyingi hivyo tunaendelea kufanyia kazi wakati kwa wakati ili kuboresha na watu wapate uhakika wa umeme wakati wote”,Amesema Kapinga.
Naye,Meneja wa kituo cha kupoza umeme Newton Mwakifwamba amesema utekelezaji wa mradi kituo cha kupoza umeme umefikia asilimia 93.7 huku ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme kutoka JNHPP hadi chalinze ukiwa umefikia asilimia 99.5 wakati ujenzi kituo cha kuendeshea mitambo kikiwa kimekamilika kwa asilimia 100.
Amesema mpaka sasa mradi huo umefanikiwa kusafirisha Megawati 235 kutoka bwawa la JNHPP kwenda Chalinze na kuziingiza kwe gridi ya Taifa.
“Miradi hii imewezesha kukamilika kwa miundombinu wezeshi ya kupokea umeme zaidi na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa ambapo umeme huu umefanikiwa kumaliza mgao wa umeme”,Amesema Mwakifwamba.
Mradi wa huu umegarimu kiasi cha shilingi bilioni 158 kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme na shilingi Bilioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme chalinze ambapo miradi hiyo ilianza 2021.