*Asema Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) itawanyanyua Wachimbaji Vijana na Wanawake*
*Awataka vijana kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo ya Halmashauri
Longido, Arusha.
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwepo ya Madini kama ajira mbadala na namna ya kujikwamua kiuchumi wao binafsi na familia zao sambamba na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Amesema hayo leo Mei 17, 2024, Wilayani Longido Mkoani Arusha wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana wilayani humo, ambalo limelenga kuwasaidia vijana kufahamu fursa zilizopo katika sekta za madini, kilimo, ufugaji pamoja na mikopo ya Halmashauri kwa Vikundi ya Wanawake, Vijana na Walemavu.
Dkt. Kiruswa amesema, kutokana na changamoto zilizopo katika soko la ajira hivi sasa ulimwenguni kote, ni wakati wa vijana kuhamisha fikra na nguvu zao katika ajira mbadala na kwamba fursa zilizopo katika Sekta mbalimbali kama vile Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) pamoja na Sekta Binafsi zinatoa nafasi kwa vijana wenye elimu na waliyokosa fursa za kusoma kufikia vyuo vya kati na vyuo vikuu.
“Mataminio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vijana wanachamgamkia fursa za ajira mbadala ili kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta binafsi na ametuelekeza kuwasadia vijana kufahamu fursa hizo na kuwawezesha kimbinu pamoja na mitaji kufikia ndoto zao” amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amewataka vijana kuunda vikundi ili wanufaike na mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa ajili ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Walemavu ili kujikwamua kiuchumi kwa kuwa Serikali imeshafanyia marekebisho namna ya usimamizi wa mikopo hiyo na mwaka ujao wa fedha itaanza kutolewa kwa vikundi hivyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Marko Ng’umbi amewataka vijana kuzingatia mafunzo na maarifa waliyoyapata kwenye kongamano hilo na kuyafanyia kazi kwa kuwa ni fursa ya kipekee kwao itakayowasaidia kuwafungua kifikra na hatimaye kujiajiri.
Akitoa wasilisho kuhusu Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT), Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Ushiriki wa Watanzania Kwenye Miradi ya Madini (Local Content) pamoja na Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) Maruvuko Msechu amesema kuwa programu hiyo imeandaliwa na Wizara ya Madini kwa lengo la kuhakikisha Makundi ya Wanawake na Vijana yanafaidika na Rasilimali Madini yaliyopo nchini.
Amesema kuwa kupitia MBT, Wizara inalenga kuwapatia vijana na wakinamama kwenye vikundi leseni katika maeneo ya uchimbaji pamoja na Wachimbaji kunufaika na vitendea kazi ikiwemo magari, vifaa na mitambo ya uchimbaji.
Ameongeza kuwa matarajio ya Programu ni kuchochea ukuaji wa Sekta ya Madini, kuongeza ajira kwa Watanzania, kuwajengea uwezo vijana katika kushiriki kwenye uchumi wa Madini na uwekezaji katika Sekta ya Madini, Ushiriki kwa vijana kwenye maamuzi na Usimamizi wa Sheria,
Pia, Msechu amesema kuwa MBT inatarajiwa kuongeza Ushiriki wa Watanzania katika shughuli za madini na Uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, kuwajengea uwezo vijana na wanawake wa Tanzania kwenye biashara ya madini kupitia fursa za uwepo wa madini ya aina mbalimbali Tanzania.