Wananchi wa Kata ya Ndalambo wilayani Momba wametakiwa kuwapa malezi bora watoto wao ili kutengeneza kizazi bora kwa maendeleo ya taifa.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Agustino Senga, Mei 17, 2024 wakati alipokuwa anawajengea uelewa wazazi kuhusu umuhimu wa malezi bora kwa watoto na kuwalinda watoto wao ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu sambamba na vitendo vya mmomonyoko wa maadili.
Kamanda Senga alisema kuwa, “malezi bora kwa watoto yanaanza na maelewano katika ndoa kama mnaishi vizuri bila migogoro kwenye ndoa zenu bila shaka watoto wenu watajifunza tabia njema na watakuwa wazazi wazuri wa watoto wao katika maisha yao ya baadae na tutapata kizazi bora ambacho kinafata mila na desturi za Mtanzania”
Kamanda Senga aliongeza kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuwa karibu na watoto ili kupata taarifa wanazofanyiwa wakiwa shuleni kwenye michezo na hata nyumbani ili kuzishunghulikia kwa haraka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa lengo la kutokomeza vitendo viovu katika jamii na hapo tutakuwa tumetengeneza kizazi bora kwa maendeleo ya taifa letu.