JAMII imetakiwa kukata Bima ili kujikinga na majanga mbalimbali ikiwemo ulemavu wa kudumu.
Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dk Baghayo Saqware wakati wa uzinduzi wa Bima ya ADABIMA na Saccos Schemes Credit Life inayotolewa na Tanzania Commercial Bank (TCB) kwa kishirikiana na Kampuni ya Metro Life Assurance.
Dk Baghayo amesema kuwa mtu akiwa na bima anakuwa na uhakika wa kutokurudi nyuma katika maendeleo kutokana na majanga mbalimbali katika kazi zake za kila siku kwa kuwa ikitokea bima yake itamsaidia.
“Majanga ya vifo, ukemavu na mengine yanaweza kutokea mtu yeyote au mzazi yeyote ni vyema kujipanga na kununua bidhaa za bima ili tusivuruge ndoto na kiu za watoto wetu au familia zetu”, alisema Dk Baghayo.
Amesema kutokana na maelekezo na usimamizi mzuri wa serikali chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan soko la bima limeendelea kuimarika nchini.
Dk Baghayo amesema kuwa mwaka 2020/21 soko lilikuwa kwa asilimia 26 na kubainisha kuwa soko limeeendelea kukua na ripoti itakayotolewa mwezi Oktoba itaonesha hali ya soko kwa mwaka huu.
Amesema kukuwa kwa soko kumesababisha ada za bima kuongezeka kutoka Bilioni 893 mwaka 2020/21 na kufikia Trioni 1.2 mwaka 2020/22.
“Tunategemea ripoti ya 2020/23 tuwe na matrioni mengi zaidi yameongezeka, matarajio yetu mamlaka na serikali kwa ujumla ni kuona soko linatanuka na kuwafikia wananchi wengi” alisema.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Jema Msuya amesema kuwa bima ya ADABIMA itasaidia watoto kufikia ndoto zao baada ya wazazi au walezi wao kufariki kwa kiwa bima itaendelea kimlipia gharama za masomo kuanzia shule ya msingi hadi chuo.
Amesema kuwa ndoto nyingi za watoto zimekuwa zikiishia njiani baada ya wazazi wao kufariki au kupata changamoto ya ulemavu wa kudumu.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Metro Life Assurance, Amani Boma amesema kuwa bidhaa zilizozinduliwa zitafufua matumaini na ndoto za watu wengi na kuitaka jamii kujiunga na bima hizo.
Awali akizingumza katika uzinduzi huo Ofisa Mtendaji wa Bima Benki, Francis Kaaya amesema bima hizo zitawapa wateja usalama wa fedha na na zitalea ndoto na matarajio ya wateja.