Mkuu wa mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amewaagiza wadau wa afya wa mkoani humo kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili kulipa madeni yaliyopo MSD na kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya vituoni.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi amesema hayo alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi cha cha wadau na wateja wa MSD mkoa wa Katavi wanaohudumiwa na MSD kanda ya Tabora.
Aidha ameipongeza menejimenti ya MSD kwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, kwani kiwango kimekuwa kikiongezeka siku hadi siku.
Kwa upande mwingine amewaagiza waganga Wakuu wa Wilaya na Wafamasia kufuatilia matumizi sahihi ya bidhaa za afya kwenye kila ngazi ili kuhakikisha usimamizi mzuri unazingatiwa.
Naye Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji kutoka MSD Victor Sungusia, ameeleza maboresho mbalimbali yaliyofanywa na MSD kiutendaji, ikiwa ni pamoja na ongezeko la kukidhi mahitaji ya wateja kutoka asilimia 40 mwaka 2021/2022 hadi kufikia asilimia 86 sasa.
Aidha amebainisha juhudi mbalimbali za MSD katika kuongeza maeneo ya Uhifadhi katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na jitihada za uzalishaji wa bidhaa za afya nchini.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Waganga wakuu wa Halmashauri, wafamasia, wataalam wa maabara, Waganga Wafawidhi na Mameneja wa Hospitali za wilaya za mkoa wa Katavi.