Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kitaendelea kusalia katika Bahari ya Hindi katika eneo kati ya Madagascar na visiwa vya Shelisheli kwa siku nne zijazo kabla ya kuanza kupungua nguvu.
Aidha, kutokana na umbali kutoka nchini, kimbunga hicho hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja katika kusababisha ongezeko la mvua nchini. Hata hivyo vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa vinaweza kujitokeza katika Bahari ya Hindi.
USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.