VIONGOZI wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi wametakiwa kuipa kipaumbele ajenda ya Lishe ndio ajenda kuu kwenye kila mkutano katika wilaya ya Nachingwea.
Akizungumza wakati wa kikao cha lishe ,Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo aliwataka watendaji wote wa kata katika wilaya hiyo kuhakikisha wanaipa kipaumbele ajenda ya Lishe ili kuwezesha watoto wanakuwa katika misingi inayotakiwa.
Moyo alitangaza kila shule lazima walime bustani za mboga mboga kwa ajili ya kutoa elimu ya lishe bora kwa faida ya taifa na kila mtendaji aliyesajiliwa na serikali lazima asimamie suala la lishe popote pale alipo.
Moyo aliwaambia watendaji wa kata kutoa elimu ya lishe ili kuwa na kizazi bora chenye uwezo wa kufikiri kwa kina na kuleta maendeleo kwa taifa kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Mtoto asipokuwa na lishe bora basi taifa litakuja kuongozwa na viongozi wasiokuwa na uwezo na kulipeleka taifa sehemu isiyo takiwa”
Moyo alimalizia kwa kusema kuwa mtendaji yoyote asipotezeleza ajenda ya lishe atafute sehemu nyingine ya kufanya kazi maana agenda ya lishe ni ajenda ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mhandisi Chionda Kawawa aliwataka watendaji wote kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaopuuza ajenda ya Lishe.
Mhandisi Kawawa alisema kuwa watendaji wanatakiwa kuacha uzembe mara moja maana haiwezekani ndani ya miezi mitatu ukashindwa kufanya tukio la kutoa elimu ya lishe katika kata yako.
Alitoa ovyo kali kwa mtendaji yoyote yule atakaye shindwa kuibeba ajenda ya Lishe basi atawajibika kwa mujibu wa kanuni na sheria za Halmashauri.