Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya familia duniani ambayo kimkoa yamefanyika kijiji cha Suluti wilayani Namtumbo.
baadhi ya wananchi wa kijiji cha Suluti wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakiwa kwenye maadhimisho ya kimataifa ya siku ya familia ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
………………………..
Na Albano Midelo,Namtumbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesikitishwa na
hali isiyoridhisha ya malezi na uangalizi wa mtoto.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia ambayo
kimkoa yamefanyika Kijiji cha Suluti wilayani Namtumbo,amesema wazazi
na walezi wengi wamekuwa hawatimizi ipasavyo majukumu ya malezi na
kusababisha malezi ya upande mmoja.
“Takwimu kutoka ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa kwa kipindi cha kuanzia
Januari hadi Desemba 2023 zinaonesha kuwa jumla ya mashauri 3,441
yalipokelewa na kushughulikiwa ambapo mashauri 1,611 sawa na asilimia
47 yalihusu matunzo ya watoto,mashauri 831 sawa na asilimia 24 yalihusu
matatizo ya ndoa na mashauri 969 sawa na asilimia 29 yalihusu mashauri
nje ya ndoa’’,alisema Kanali Abbas.
Amebainisha kuwa Ofisi ya Ustawi wa Jamii imekuwa ikipokea kesi za
matunzo ya Watoto na malalamiko yanayoelekezwa upande wa akinababa.
Ametoa rai kwa wazazi na walezi ambao wamefarakana kutambua kuwa
mtoto bado anastahili malezi yaliyo bora hivyo ni vema kuweka mpango
mzuri wa kumlea mtoto ili asiathirike kimalezi na kwamba wazazi wajitahidi
kuvumiliana ili kuepusha kuachana kusiko kwa lazima hivyo kumuathiri
mtoto.
Akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia Mariam
Juma ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma ameitaja kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema
tukubali tofauti zetu kwenye familia,kuimarisha malezi ya Watoto,
inawakumbusha wazazi na walezi kuweka kando tofauti zao na kuangalia
malezi na huduma zinazostahili kwenye familia.
Juma amebainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba
2023 mashauri 2,859 ya ukatili yalitolewa taarifa na kushughulikiwa katika
ofisi za ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma na kwamba mashauri 121
yalifikishwa mahakamani.
Hata hivyo amesema mashauri 77 sawa na asilimia 63.6 yalihukumiwa,kati
ya mashauri 1,580 ya Watoto,mashauri 1050 sawa na asilimia 66.6 yaliwahusu wasichana wakati mashauri 1,279 ya watu wazima,mashauri
1,030 sawa asilimia 80.5 yaliwahusu wanawake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya
amesema wazazi wote wawili wanatakiwa kuwajibika kwa malezi ya familia
ili fahari ya mtoto na mafanikio yake yawe kwa wazazi wote wawili kwa
kuwa mtoto ni wa wazazi wote.
Amewashauri wazazi na walezi kuwalea Watoto kwa misingi
inayompendekeza Mwenyezi Mungu na kuheshimu sheria za nchi,
Hata hivyo Malenya amesisitiza upendo kwa familia ambao unafanikisha
malezi bora kwa familia na kutahadharisha kuwa wazazi na walezi
wasipoungana kwa dhamira hawataweza kutimiza ndoto za Watoto wao.
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa Mei 20,1993 lilitenga siku
maalum ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia lengo likiwa ni
kutambua nafasi ya familia katika jamii.