Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor
Mpango akifanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa
Canada Mhe. Ahmed Hussein Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor
Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa
wa Canada Mhe. Ahmed Hussein mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika
Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor
Mpango akiagana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe.
Ahmed Hussein mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es
Salaam tarehe 16 Mei 2024.
……………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor
Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo ya
Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussen Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini
uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yake na Canada na kuishukuru kwa
kuinguka mkono Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu,
Biashara na Uwekezaji, Kilimo pamoja na Ulinzi na Usalama. Amesema Mataifa
haya mawili yameendelea kushirikiana kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Madola
pamoja na Umoja wa Mataifa.
Makamu wa Rais ameikaribisha Canada kushirikiana na Tanzania katika
kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutumia uzoefu wa nchi hiyo pamoja na
kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo. Pia ameishukuru Serikali ya Canada
kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya nishati safi
ya kupikia.
Amesema kuunga mkono jitihada hizo kutaharakisha wananchi wa
Tanzania kuondokana na nishati isiyofaa ya kupikia na kufikia malengo ya
mkakati wa kitaifa wa kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo
mwaka 2034.
Makamu wa Rais amesema kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi zaidi
kuwekeza kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza katika kuimarisha
uchumi pamoja na kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara
kwa kufanya mageuzi ya kitaasisi, kisera na kuimarisha utawala wa
demokrasia.
Amesema ni muhimu kufanya kazi pamoja katika kuharakisha
majadiliano ya kuboresha Mkataba wenye usawa na maslahi kwa pande zote
mbili wa kinga katika uwekezaji baina ya Canada na Tanzania (FIPA).
Aidha amesema Serikali ya Canada inaweza kushirikiana zaidi na Tanzania
katika sekta ya afya kwa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa, kuwekeza
katika makao makuu ya nchi Dodoma katika ujenzi wa miundombinu, udhibiti
wa taka ngumu, viwanja vya michezo pamoja na mazao ya mbogamboga.
Vilevile Makamu wa Rais ameishukuru serikali ya Canada kwa kuiunga mkono
Tanzania dozi milioni 22 za vitamini A pamoja na kutangaza ahadi ya dola
milioni 25 katika mradi wa kilimo rafiki kwa mazingira na kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed
Hussen amesema uhusiano wa Tanzania na Canada ni wa muda mrefu katika
hali zote ambao umeendelea kuimarika.
Amesema katika wakati huu ambao
Tanzania imefikia uchumi wa kati wa chini ni muda muafaka wa kuongeza
ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
Amesema katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi
Canada inatambua umuhimu wa kufanya kazi pamoja ili kuondoa athari kwa
wananchi. Ametoa pole kwa serikali na wananchi wa Tanzania na familia
zilizoathirika na kimbunga hidaya pamoja na mvua za el nino zilizopolekea
madhara makubwa.
Ameongeza kwamba Canada inaendesha miradi mbalimbali nchini Tanzania
ikiwemo ya kuwajengea uwezo wananchi katika kuhimili mabadiliko ya
tabianchi pamoja na kilimo rafiki kwa mazingira.
Waziri Hussen amesema Canada itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
sekta mbalimbali ikiwemo mazingira, afya, lishe na elimu.