Mshauri wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Taasisi ya Forumcc, Rebecca Muna.
…………
NA VICTOR MAKINDA. MOROGORO
Wito umetolewa kwa wananchi kuongeza uelewa na utayari katika kujiandaa kabla na kujua namna ya kufanya wakati wanapokumbwa na majanga ya mafuriko ili kupunguza athari za kijamii na kiuchumi.
Wito huo umetolewa jana na Mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Asasi inayohusika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi (ForumCC Tanzania) Rebecca Muna, wakati akizungumza na waathirika wa mafuriko wa kata za Lukobe na Kihonda, Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya mafuriko na kufahamu hatua za kuchukua pindi wanapokubwa na mafuriko.
Rebecca alisema kuwa wananchi wana uelewa mdogo kuhusu majanga hususani janga la mafuriko hivyo taasisi ya Forumcc imeona kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi wote hususani wale walioathiriwa na mafuriko ili waweze kuongeza uelewa na uhimili wa athari zilizotokana na mafuriko.
“Mabadiliko ya tabia yameleta athari za mvua kubwa na za Elnino hatimaye kusababisha mafuriko katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ya nchi, yapo maeneo yamekumbwa na mafuriko ya zaidi ya mara moja na kusababisha hasara kubwa ya kuharibika kwa mali sambamba na vifo”. Alisema Rebecca.
Muna aliongeza kusema moja ya njia ya kujikinga na majanga ya mafuriko ni wananchi kusikiliza na kuzichukulia hatua taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini.
“Tunatakiwa kuwa makini kufuatilia taarifa za hali ya hewa Sambamba na kufuata ushauri wataalam jinsi yakuepukana na matokeo mabaya yanayosababishwa na mvua kubwa, upepo na vimbunga.” Anasema.
Alisema kuwa ni vema wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama katika maeneo hayo kwa kuwa kila inaponyesha mvua kubwa maeneo hayo hukumbwa na mafuriko.
Aliongeza kuwa taasisi ya Forumecc kwa kushirikiana na ActionAid, Plan international, CAN Tanzania kwa ufadhili Start Fund wameweza kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo mablanketi na vyakula kwa waathirika wa mafuriko katika wilaya za Malinyi, Ulanga, Kilombero na Manispaa ya Morogoro.