Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (wa nne kulia), akigonga kengele kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kuashiria kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika Ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika Ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika Ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akitoa salamu za Wizara katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika Ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma
Manaibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo (kulia), Bw. Elija Mwandumbya (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Agnes Meena, wakifuatilia kwa karibu hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), katika Ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
………………………
Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amezielekeza Taasisi za Serikali kutumia utaratibu wa Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing) badala ya kutegemea Bajeti ya Serikali pekee.
Agizo hilo limetolewa kwa niaba yake na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.
Mhe. Bashungwa alisema kuwa kugharamia miradi ya maendeleo kwa njia mbadala kutaiwezesha Serikali kujielekeza katika maeneo mengi zaidi na kuboresha maisha ya watanzania.
“Fedha zote zilizohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Tanga UWASA hivi sasa zimepatikana, Wizara ya Fedha itaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa mafanikio kama ilivyopangwa”, alisema Mhe. Bashungwa.
Alisema kuwa Hatifungani hiyo inathamani ya shilingi bilioni 53.1 ikiwa ni ya kwanza kutolewa na Taasisi ya Serikali kwa utaratibu wa ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa njia mbadala (APF).
Mhe. Bashungwa alisema kuwa kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa tarehe 30 Aprili, 2024 na Tanga UWASA na kuidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inaonyesha jumla ya shilingi bilioni 54.72, zimekusanywa ikiwa ni juu ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 53.12 sawa na ufanisi wa asimilia 103, ambapo fedha hizo zitawezesha kuboresha miundombinu ya maji na kuongeza uzalishaji maji mara mbili ya uwezo uliopo sasa wa lita za ujazo 30,000 hadi lita za ujazo 60,000 na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.
Aidha aliwapongeza wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha tukio hilo, na kusisitiza taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano huo.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso, alisema kuwa miaka ya nyuma Wizara ya Maji ilikuwa Wizara ya kero na lawama lakini kwa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mageuzi makubwa ambayo yamesaidia kuondoa adha ya maji kwa kiwango kikubwa.
Alisema ni nadra sana kuona taasisi ya umma inafanya jambo kubwa kama hilo la kuorodhedha Hatifungani kwenye masoko ya Hisa jambo linaloifanya Tanzania kuwa darasa kwa nchi nyingi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa tukio hilo ni muhimu kwa kuwa linatekeleza azma ya Serikali ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia vyanzo bunifu, hivyo kama mlipaji Mkuu wa Serikali imempa faraja kubwa kuona kwamba kuna ubunifu katika kupatikana kwa vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinatoa unafuu katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya nchi, mitaji inayopatikana kutoka kwenye mifumo mbalimbali nje ya bajeti ya Serikali ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam, Bi. Mary Mniwasa, alisema kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, ukubwa wa Soko la Hisa umeongezeka kwa Kampuni za Tanzania ambapo uwekezaji umeongezeka kutoka shilingi tirioni 9.2 kwa kipindi cha Machi, 2021 hadi shilingi tirioni 11.8 kwa kipindi kilichoishia Machi, 2024.